📌Ni kwa miradi inayozalisha chini ya Megawati 10
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu ametoa wito kwa waendelezaji wa miradi ya nishati jadidifu kote nchini kuchangamkia fursa za uwezeshwaji zinazotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kuwa na miradi yenye tija kwa Taifa.
Ametoa wito huo Juni 19, 2025 akiwa kwenye ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa kuzalisha umeme wa Mwenga wa megawati nne unaomilikiwa na Kampuni ya Mwenga Hydro Limited kwa kutumia maporomoko ya Mto Mwenga katika Kijiji cha Ifwagi, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.
"Kwenye eneo hili la nishati jadidifu fursa zilizopo ni nyingi, Tanzania ni kubwa na imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi na bado hazijatumika ipasavyo; tunahitaji waendelezaji wengi wa miradi ya kuzalisha umeme kwa upepo, joto ardhi, jua na maporomoko ya maji kujitokeza ili kuwezeshwa na REA kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme nchini," alisema Mhe. Balozi Kingu.
Alisisitiza kuwa waendelezaji wa miradi ya nishati jadidifu ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya Taifa hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa.
Akiwasilisha taarifa ya Mradi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Rift Valley Energy kampuni mama ya Mwenga Hydro Limited, Michael Gratwicke aliishukuru REA kwa uwezeshwaji mkubwa iliyofanya katika mradi huo.
"Tunaishukuru REA kwani leo hii tunahudumia takriban kaya 10,000 ndani ya vijiji 32 kutokana na uwezeshwaji wa REA; tusingefika hapa kama isingekuwa uwezeshwaji huu," alisema Gratwicke.
Akizungumza kuhusiana na uwezeshwaji kwa ujumla, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema REA ilitoa ruzuku ya takriban shilingi bilioni 23 kuendeleza mradi huo.
Alisema kuwa Wakala unatoa kipaumbele kwenye ujenzi wa miradi ya nishati jadidifu nchini ili kusaidia utunzaji wa mazingira, kuboresha upatikanaji wa umeme, kuongeza uzalishaji wa umeme unaotokana na nishati Jadidifu pamoja na kutoa ajira kupitia miradi hiyo.






Comments
Post a Comment