Na Ada Ouko, GMTV
SERIKALI mkoani Mara kwa kushirikiana na Uongozi wa Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo Wilayani Tarime wamefungua mafunzo maalumu kwa wachimbaji wadogo yatakayowawezesha kuendesha shughuli zao kwa tija na kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, wakati akifungua mafunzo hayo Juni 20, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka alisema mpango wa mafunzo hayo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa madini Antony Mavunde aliyefanya ziara mwezi May mwaka huu mkoani humo.
" May mwaka huu Waziri wa madini alikuja hapa Nyamongo kwa ajili ya kuwakabidhi leseni vikundi vya vijana, ambapo jumla ya vikundi 48, na vijana 1736 walikabidhiwa leseni za uchimbaji kwa lengo la kuwawezesha kunufaika na rasilimali zitokanazo na sekta ya madini"Alisema Chikoka.
Aidha aliwataka vijana na wanawake wanaonufaika na mradi huo kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo , Sambamba na hilo alitoa rai kwa Taasisi zinazohusika kusimamia vikundi hivyo ikiwemo ofisi ya madini ya mkoa huo na STAMICO kuendelea kuwasimamia kwa ukaribu hadi watakapo imarika katika kukuza uchumi wao binafsi na kuongeza pato la Taifa.
Afisa madini mkaazi wa mkoa huo Amini Msuya alisema mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku 14 ambapo yalianza rasmi Juni 21, 2025, ambapo yatahusisha mada mbalimbali ambazo zitawajengea uwezo kwenye uchimbaji wa madini, ikiwemo matumizi ya fedha,uhifadhi wa mazingira, sheria ya madini, Biashara ya madini.
"Hii ndio ya utekelezaji wa mradi wa baada ya vijana hao kupewa leseni, utekelezaji wa mradi huu ulipitia katika hatua zifuatazo, kwanza tulisajili vijana na akina mama wanaohitaji kuingia kwenye mradi, pili waliosajiliwa wakaunda vikundi,tatu Serikali ikawakabidhi leseni vikundi vilivyosajiliwa na sasa tuko hatua ya nne ambayo ni kuwajengea uwezo vijana walioko kwenye vikundi kabla hawajaanza rasmi shughuli za uchimbaji" Alisema Msuya.
Kwa upande wake Afisa mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Frances Uhadi alisema mafunzo hayo ni jitihada za mfuko wa dhamana ya North Mara ili kuhakikisha Sekta ya madini kwa wachimbaji wadogo inakuwa kwa tija zaidi, Ikizingatia usalama, uendelevu wa mazingira, usimamizi wa vikundi.
"Tutaendelea kuunga mkono kwa njia mbalimbali ilikuhakikisha sekta ya madini inazidi kuwainua vijana hususani wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara, Naomba niwahimize wachimbaji kuwa na uaminifu,waadilifu na waendelee kujifunza ili kuboresha shughuli zao za uchimbaji"Alisema.
Mkuu wa chuo cha Veta mkoani humo, Martin Mollel alisema baada ya wachimbaji hao kupata mafunzo yao uongozi wa chuo hicho utawafuatilia kwa ukaribu na kuwapa elimu mbalimbali ya matumizi ya mashine za kisasa katika shughuli zao sambamba na hio watawapa elimu ya kujikinga na majanga yatokanayo na shughuli za migodi.
" Veta tumekuja na mashine nne ambazo zitamuwezesha mchimbaji kuchimba vizuri na kufanikiwa kwa haraka miongoni mwa mashine hizo ni mashine ya kusaga mawe mabichi na makavu kwa wakati mmoka,tunayo pia mashine ya kukamatisha dhahabu ili kuepusha kukamata dhahabu kwa mkono hali ambayo inahatarisha maisha ya mchimbaji" alisema.
Miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo, Mchimbaji mdogo na Mkurugenzi wa kampuni ya (SoyaOne Limited) Chacha Soya aliishukuru serikali kwa kuwaletea mafunzo hayo na kusema matumizi sahihi ya leseni walizopewa wachimbaji hao yatawakwamua kutoka kwenye umaskini na kukuza uchumi wa serikali.













Comments
Post a Comment