Askari 238 Wahitimu Mafunzo Jeshi La Uhifadhi

GEORGE MARATO TV
0


*Na. Happiness Sam- Katavi*

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia masuala ya Uhifadhi Kamishna wa Polisi (CP) Benedict Wakulyamba,Jana Juni 10, 2025 amefunga rasmi mafunzo kwa Maafisa na Askari wapya 238 wa Jeshi la Uhifadhi na Misitu kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika Kituo Cha Mafunzo cha Jeshi hilo kilichopo Mlele mkoani Katavi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo CP Wakulyamba alisema, “mafunzo haya mliyoyapata ni muhimu kuyatekeleza kwa vitendo pamoja na kuwa na ushirikiano mzuri kazini kwa lengo la kuboresha utendaji  kazi na kuyaishi yale  yote mliyofundishwa ili kuchochea uwajibikaji”.

Aidha, CP Wakulyamba alieleza kuwa mafunzo hayo hayawezi kuwa na maana yoyote endapo yatabaki kama nadharia isiyofanyiwa kazi, bali ni lazima yatumiwe kama nyenzo ya kuchochea uwajibikaji, maadili mema, na nidhamu kazini na kuwataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mfano bora wa kuigwa katika maeneo yao ya kazi kwa kutumia maarifa waliyoyapata ili kuleta mabadiliko chanya katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Sambamba na hayo, CP Wakulyamba alitoa pongezi kwa Maafisa na Askari waliohitimu mafunzo hayo na kuongeza kuwa elimu na ujuzi walioupata ukawe nguzo imara ya kuwajengea  maadili, uaminifu na unyenyekevu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya Watanzania wote.

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Godwell Meing’ataki, Mkuu wa Kanda ya Kusini, aliwapongeza wakufunzi na wote walioshiriki kufanikisha mafunzo hayo, akisisitiza kuwa juhudi na kujitolea kwao kumechangia kuandaa Maafisa na Askari wenye ari, morali, na utayari wa kulitumikia Taifa kwa uaminifu na uzalendo.

Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza, Bernadeta Aloyce ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Mafunzo Mlele alisema, “ tumetoa mafunzo mbalimbali kwa Maafisa na Askari wapya wa Jeshi la Uhifadhi, mafunzo hayo yalihusisha uelewa wa sheria za kijeshi, uongozi na upangaji wa kazi za kila siku, pamoja na ustawi wa masuala ya uhifadhi na utalii na tumetoa mafunzo hayo kwa njia ya nadharia na vitendo ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi”.

Hafla ya kuhitimisha mafunzo ya nadharia na vitendo kwa Maafisa na Askari 238 wa Jeshi la Uhifadhi na Misitu imefanyika Jana katika Kituo cha Mafunzo Mlele, mkoani Katavi na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia masuala ya Uhifadhi, CP Benedict Wakulyamba, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Fidelis Kapalata ambaye ni Mratibu wa Jeshi la Uhifadhi Wizara ya Maliasili na Utalii, Menejimenti ya TANAPA pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top