BARIADI, Simiyu
Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew, ametangaza kuwa endapo Jimbo hilo litagawanywa rasmi, atagombea tena Ubunge kupitia Jimbo la Bariadi Vijijini – eneo analotokea na analosema lina uhitaji mkubwa wa maendeleo ya karibu.
Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Bariadi uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Bariadi Alliance, Mhandisi Kundo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 mbele ya wajumbe wa mkutano huo, huku akitumia jukwaa hilo kueleza dhamira yake ya kuendelea kulitumikia Taifa kupitia mzizi wake wa kijijini.
> "Kuna mkakati wa kugawa Jimbo la Bariadi kutokana na ukubwa wake wa kata 31. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imefika kukusanya maoni na sisi kama viongozi tumeonyesha nia njema ya kupendekeza mgawanyo huo ili kurahisisha shughuli za maendeleo na kuwasogezea wananchi huduma muhimu," alisema Mhandisi Kundo.
Aidha, alieleza wazi kuwa iwapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataridhia ombi hilo, basi yeye atarejea nyumbani na kugombea Ubunge wa Bariadi Vijijini.
> “Mimi ni mzaliwa wa Bariadi Vijijini, ninajua changamoto za huko, najua ndoto za wananchi wa huko. Nikipewa fursa, nitarejea nyumbani kuendeleza mapambano ya maendeleo kwa vitendo. Mkataa kwao ni mtumwa – na mimi si mtumwa,” alisema kwa msisitizo.
Kauli hiyo imeibua msisimko mkubwa kwa wajumbe wa mkutano na kutafsiriwa kama ishara ya ujasiri, uzalendo, na dhamira ya dhati ya kiongozi huyo kijana kuendelea kushikamana na wananchi wake waliomlea na kumwamini.









