Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ameonyesha kuunga mkono hatua ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuzuia wanaharakati na mawakili wa Kenya kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania.
Muhoozi amemsifu Rais Suluhu kwa kuwa kiongozi mwenye maamuzi thabiti, akisema kuwa anazidi kuwa mmoja wa viongozi anaowapenda barani Afrika.
“Mama Samia Suluhu, rais wa Tanzania, ni miongoni mwa viongozi ninaowaenzi barani afrika. Ni mwenye msimamo dhabiti na hapendi mambo ya kipuuzi. Asante sana Mama”-, alisema katika akaunti yake ya X.
Kauli yake inajiri baada ya wanaharakati wa Kenya, akiwemo Martha Karua na Willy Mutunga, kuzuiwa kuingia Tanzania wakitaka kufuatilia kesi ya Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi na uhaini.
Rais Dkt. Samia Suluhu amesisitiza kuwa Tanzania haitaruhusu wageni kuingilia masuala yake ya ndani, akisema kuwa nchi hiyo si “shamba la bibi” ambapo kila mtu anaweza kusema au kufanya anavyotaka bila mipaka.





Comments
Post a Comment