Na Angela Sebastian; Bukoba
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa ajili ya kuendeleza miradi mikubwa ya soko jipya la kisasa na stedi ya mabasi yaendayo mikoani.
Sima ametoa shukrani hizo Mei 27 mwaka huu wakati akikagua maeneo ya mradi wa ujenzi wa soko ambao uko katika hatua za mwanzo ambapo ni ubomoaji wa majengo ya zamani na kusafisha eneo lilipokuwa soko la zamani ili kuwa tayali kwa kuanza ujenzi rasmi.
"Ujenzi huu wa soko umekuwa kizunguzungu kwa miaka mingi lakini kutokana na upendo kwa wananchi anaouonyesha Dk.Samia Suluhu Hassan kutaka kuupendezesha mji wa Bukoba na kuleta huduma karibu kwa wananchi ametuletea shilingi bilioni 19 ili soko hili likamilike na standi kuu tunamshukuru sana" amesema Sima
Amesema kuwa miradi hiyo ni moja ya miradi ya Tactics ambayo inajengwa nchi nzima na sasa mradi wa soko kuu mkandarasi mshauri tayali anaendelea na kazi yake.
Amewashukuru wananchi hususani wafanyabiashara katika soko hilo ambao waliamua kuhama wenyewe kwa hiari bila kuzusha vurugu na kukubali kwenda katika eneo ambalo Serikali imewatengea ili wafanye biashara kuwa hiyo ni hatua ya kizalendo.
Amesema sasa wanaendelea kufanya usafi kwa kuondoa miundombinu iliyokuwepo na kisha kumkabidhi mkamdarasi eneo aweze kuanza kazi ya ujenzi muda wowote kuanzia sasa na mradi huu unaenda kukamilika kwa asilimia 100
Diwani wa Kata ya Bilele, Tawfiq Sharif, amepongeza hatua ya ubomoaji kwa kusema ni dalili ya nia thabiti ya Serikali kutekeleza Ilani ya CCM.
Wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao ndani ya soko la zamani, kama Safina Seleman, wameelezea furaha yao baada ya kuona hatua hizi za awali zitakazowezesha ujenzi wa soko safi na salama.
Pia baadhi ya wananchi wa Bukoba wamesema kuwa hatua hiyo ya awali ya ubomoaji ni dalili nzuri ya kuondoa migogoro ya muda mrefu na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha wametoa shukrani kwa Serikali kwa kuanza hatua za utekelezaji wa miradi hii muhimu ambapo utekelezaji wa miradi mikubwa ya soko la Bukoba na kituo cha mabasi unatoa matumaini mapya kwa maendeleo ya mji huu na kuonyesha dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Hatua hizi ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kuboresha maisha ya kila Mtanzania katika mji wa Bukoba.
Miradi mikubwa ya kihistoria inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi wa mji wa Bukoba. Miradi hii ni pamoja na ujenzi wa soko la kisasa la Bukoba na kituo cha mabasi yaendayo mikoani, ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yamekwama kutokana na migogoro ya kisiasa.