Na Shomari Binda-Tarime
WATUMISHI wanawake wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)mkoa wa Mara wametembelea kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha 'Angel House' kilichopo katika Wilaya ya Tarime na kutoa misaada ya vitu mbalimbali.
Katika tukio hilo la matendo ya huruma TAKUKURU imewapatia watoto hao mahitaji muhimu yakiwemo vyakula, mavazi na vifaa vya shule .
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo,Afisa wa TAKUKURU mkoa wa Mara Restituta Kessy amesema katika kusherehekea siku ya kimataifa ya wanawake duniani wameona wawafikie watoto hao kwenye kituo hicho.
Amesema ni jambo la faraja kumuona kila mtoto anakuwa na furaha wakiwemo watoto yatima na kujiona kama watoto wengine.
Afisa huyo amesema jamii inapaswa kuwa na utaratibu wa kutembelea vituo vya watoto yatima na wenye uhitaji ili kuweza kuwasaidia na kuwafanya kuwa na furaha.
Amesema zipo baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu pale unapowasaidia watoto yatima na wenye uhitaji kwa kuwa vitabu vya dini vimeeleza.
" Tumeamua kukifikia kituo hiki katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani na kutoa misaada kwa watoto wetu wapendwa.
" Tumewakabidhi vyakula, vinywaji,mavazi zikiwemo sare za shule ni imani itasaidia kwa kipindi furani lakini jamii inapaswa kuwa na utaratibu wa kutembelea vituo hivi",amesema.
Mlezi wa kituo hicho Peter Emmanuel ameishukuru TAKUKURU kwa kujali wahitaji pamoja na kuwatia moyo watoto waliopo kwenye kituo hicho kutokana na msaada waliopokea.
Peter amewatakia watumishi hao wanawake wa TAKUKURU mkoa wa Mara mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi na kuwakaribisha tena kutembelea kituo hicho.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake inasema "Wanawake na wasichana 2025:
Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji".




Comments
Post a Comment