Na MASHAKA MHANDO, Tanga
WAISLAMU nchini wametakiwa kuendeleza matendo mema ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuyaishi hata baada mfungo huo kumalizika.
Akizungumza katika Swala ya Eid el Fitr katika msikiti wa Chumbageni Jijini Tanga, Sheikh Mussa Zubeir alisema Watanzania hasa wa dini ya Kiislamu waendelee kufanya mema hata baada ya kumaliza kwa Ramadhani.
Alisema waumini wa dini hiyo kama waliweza kujizuia na mambo yasiyo mpendeza mungu katika kipindi chote Cha mfungo huo hawana budi kuendeleza matendo hayo hata baada ya mfungo kwisha.
Naye Sheikh Aziz Yunus wa msikiti wa Majengo mjini Muheza maarufu msikiti wa Mwalimu Ali, alisema kuwa Watanzania waendelee kulinda amani kama ambavyo wamemaliza funga zao kwa amani.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA, alipopewa nafasi ya kuzungumza katika msikiti huo aliwataka Watanzania kuendeleza Umoja na mshikamano na kuyaishi yale mema walivyokuwa wakiyafanya wakati wa Ramadhani.
Alisema Waislamu waendelee kujenga mashirikiano lakini pia wanapoendelea na ibada kama ambavyo walikuwa wakifanya kwenye mfungo huo, waendelee kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuliongoza Taifa kwa amani kama ilivyo Sasa.
Naye Naibu kiongozi wa Taasisi ya Vijana ya Waislamu ya Ansar nchini, amewahimiza Waislamu nchini kujenga umoja mshikamano na udugu miongoni mwao na siyo kufarakana kama inavyojitokeza hivi sasa.
Akizungumzia kuporomoka kwa maadili, Sheikh huyo alisema wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa kwa kutokemea vitendo viovu vya watoto wao kuanzia nyumbani na ngazi ya jamii.
"Wanawake mnawaacha vijana wenu kuvaa watakavyo, kuzurura mitaani muda watakao na kujihusisha na vitendo vingine viovu halafu waume zenu wakikemea mnawajia juu," alisema.
Swala ya Idd iliongozwa na Ustadh Ammi Said huku salamu za Idd zikitolewa na Kiongozi wa Taasisi ya kiislam ya Ansaar Youth Center Sheikh, Salim Barahiyan ambaye amewataka waislamu kusherehekea Idd kwa kuepuka maovu.

.jpg)






Comments
Post a Comment