Na Shomari Binda-Musoma
BARAZA la Jumuiya ya Wanawake wa CCM ( UWT) mkoa wa Mara imempongeza Rhobi Samwelly kwa kuwa kinara wa kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia.
Pongezi hizo zimetolewa machi 20,2025 na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Nancy Msafiri kwenye kikao cha baraza hilo.
Amesema kupitia kituo chake cha Nyumba Salama kilichopo Serenveti na Butiama kwa kupokea na kuwahifadhi watoto wa kike na wasichana wanaokutana na matukio ya ukatili.
Nancy amesema Rhobi amekuwa kinara na kazi yake inaonekana na jumuiya itaendelea kumpa ushitikianl katika jitihada zake za shughuli anayoifanya.
" Tunakupongeza sana ndugu yetu Rhobi kwa kazi kubwa unayoifanya katika kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia.
" Sisi UWT mkoa wa Mara tutakupa ushirikiano wote na kushirikiana nawe kwa hii kazi njema unayoifanya na Mungu atakulipa",amesema.
Awali akitoa taarifa ya masuala ya ukatili kwenye baraza hilo Rhobi Samwelly ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kupinga Ukatili wa UWT mkoa wa Mara amesema matukio ya ukeketaji yameshuka mkoani Mara kwa asilimia 8 kutoka asilimia 10 kwa wasichana na wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49.
Kushuka kwa kiwango hicho kumetokana na juhudi za wadau mbalimbali wanaopambana na matukio ya ukatili wa kijinsi kwa kutoa elimu mkoani Mara.
Amesema kwa mujibu wa utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria ( TDHS-MIS)ya mwaka 2022-2023 unaonyesha kiwango hicho kushuka.
Rhobi amesema licha ya vitendo vya ukatili wa aina ya ukeketaji kushuka bado yapo matukio mengine ya ukatili kama vipigo,ubakaji ndoa za utotoni,mauaji na manyanyaso ya kutelekezwa na kuomba kuongezwa juhudi zaidi za kupambana na matukio hayo.
" Napenda kuwaomba viongozi wanawake ndani ya jumuiya ya UWT na wadau mbalimbali wanaopambana kupinga ukatili wa kijinsia kwa uratibu wa serikali kuendeleza juhudi za kukabiliana na ukeketaji na aina nyingine za ukatili.
" Hili ni jukumu letu sisi viongozi kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yetu ikibidi kupaza sauti kwa wasioweza kupaza sauti",amesema.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa amesema jumuiya hiyo mkoa wa Mara imeshiriki kukemea ukatili wa kijinsia wa aina zote kwa kutoa taarifa na kushirikiana na wadau mbalimbali.






Comments
Post a Comment