Na Angela Sebastian; Bukoba
SHULE ya sekondari ya Nyaishozi iliyopo Wilayani Karagwe mkoani Kagera hutoa nafasi kwa wanafunzi 12 ambao wazazi wao hawana uwezo kiuchumi lakini ni wakulima wa zao la kahawa kwa ajili ya ufadhiri kimasomo.
Mkuu wa shule hiyo Audax Gereon ameeleza hayo jana wakati akiongea na mwandishi wa habari hii baada ya kufika shuleni hapo,kwa lengo la kujua namna gani wanatatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wa shule hiyo na kuzigeuza kuwa fursa.
"Kuna watoto ambao wazazi wao ni wanaushirika lakini pengine uwezo wao ni mdogo kiuchumi ata wakiuza kahawa hawezi kuwalipia ada watoto wao hivyo tunawaleta hapa shuleni tunawapa ofa ya kusoma bure kwa ufadhili wa shule"
Anasema wanafanya hivyo kwa kufuata vigezo vya kwamba uwezo wa mwanafunzi kitaaluma ni mzuri na TASAF wanamtambua kuwa ni familia duni ambapo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita wanachukua watoto 12 kila mwaka.
Amesema waliona ni budi kutumia changamoto hiyo inayowakabili watoto wa wakulima wao ambao ni wanachama kuwa fursa kwa kuwachagua watoto sita wa kike na kiume sita kutoka Wilaya za Karagwe na Kyerwa ambao ndiyo wenye shule kupitia chama kikuu cha ushirika (KDCU) ambapo watoto hao husoma bure kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita.
Amesema kwa mwaka wanafunzi zaidi ya wanafunzi 200 wanaohitimu shuleni hapo na kutokana na uwepo wa shule hiyo ambapo wengi hupata daraja la kwanza katika mitihani yao kitaifa.
Pia wameweka mfumo rafiki wa wazazi kulipa ada kupitia Amcos zao za kahawa pale wanapouza kahawa zao hivyo imesaidia wazazi wengi kuwaleta watoto shule na kupunguza wasiosoma katika Wilaya za Karagwe,Kyerwa na mkoa mzima wa Kagera na ile ya jirani.
Aidha wazazi na wanafunzi wa shule hiyo wamepongeza jitihada hizo ambazo hutengeneza wasomi wengi na wazuri watakao jenga Taifa la kesho.
Wasema uwepo wa miundombinu ya maji,uzio,barabara nzuri na umeme na malezi bora kutoka kwa walimu wao shuleni hapo umesaidia kuwaokoa wanafunzi hao kujiepusha na matendo yasiyofaa hususani ubakaji,makundi ya uvutaji dawa za kulevya na mimba za utotoni pale walipotoka nje ya shule sambamba na kuongeza ufauru katika mitihani yao.
Hivyo wanapongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita kwa kushirikiana na uongozi wa shule hiyo kwa kuwajengea miundombinu hiyo.
Aneth Jakson ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo alisema uwepo wa huduma ya maji shuleni, imewasaidia kuepukana na kukumbana na vitendo vya ubakaji na kujiingiza katika matendo ya ushawishi wa wanaume ambapo husababisha kupata mimba za utotoni na kupoteza masomo.
"Nashukuru Serikali ya hawamu ya sita na uongozi wa shule yetu kwa ushirikiano mzuri wa kutatua changamoto zinazotukabiri,miaka iliyopita wenzetu walifuata maji nje ya shule ilisababisha kubakwa na wengine waliwalag'haiwa na wanaume kwa kuwahonga ndoo za maji, matokeo yake ni kupata mimba za utotoni,kuacha shule na kuolewa katika umri mdogo"anaeleza Aneth
Aidan Bahati ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyo anasema uwepo wa miundombinu ya maji umesaidia vijana kutotoka ovyo na kutumia muda huo kufanya mambo ya ovyo ikiwemo uvutaji wa sigara kutokana na makundi ya ovyo waliochangamana nayo huko matoni.
Pia aliipongeza juhudi za shule hiyo kwa ushawishi wa mkuu wa shule kwa kuwalea wanafunzi hao katika maadili mema ikiwemo kwa kuwajengea misingi ya kusali kila mtu kwa imani yake palepale shule ambapo, viongozi wa dini zote hufika na kuwapa mafundisho yanayowajenga katika maadili ya kumjua Mungu na kuwafanya wawe watoto wanaojitambua na kuheshimiana hari inayosababisha watumie muda mwingi kujisomea na kufauru vizuri.
Jacline Bahati ni mwanafunzi pia anasema kutokana na kujihusisha na somo la kilimo na ufugaji shuleni kwao akifunga shule anao uwezo wa kumsaidia baba yake kumfundisha namna ya kutengeneza mikahawa yake,kupanda migomba kwa njia bora zaidi ambapo inasaidia kupata mazao mengi pia anaweza kuandaa vitalu vya matunda na mbogamboga kisha kuuza na kupata fedha za kujikimu.
Naye Fulumera Levelian ambaye ni mzazi wa mwanafunzi wa kidato cha nne pia ni jirani wa shule hiyo alisema anapongeza Serikali kupitia mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa na uongozi wa shule hiyo kwa kuwajenga miundombinu mbalimbali ikiwemo uzio wa kuzunguka shule,umeme na kufunga kamera ambapo hiyo imechangia kuongeza usalama kwa watoto na walimu wao pia watoto kutotoroka ovyo kwenda kujiunga katika makundi yasiyo faa.
"Kutokuwepo maji watoto walitumia muda mrefu kufuata maji zaidi ya kilometa tano huko walikutana na vishawishi vya kila aina ambavyo viliwasababisha baadhi kuacha masomo hari iliyosababisha kuiga mitindo ya maisha na kupoteza heshima na hekima,maadili mema na kupoteza muda wa kusoma wakigombania maji na wananchi kweli sera ya kumtua mama ndoo kichwani imetimia kupitia watoto wetu"alieleza Fulumera.









Comments
Post a Comment