Mashaka Mhando, Tanga
NAIBU Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo mhe Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA, amewakabidhi Bendera ya Taifa, timu ya Tanzania 'Taifa Stars' kabla ya mchezo muhimu wa kuwania kufudhu kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco, mchezo unatarajiwa kuchezwa Machi 26, 2025.
Akizungumza Leo Machi 20, 2025 Jiji Tanga kwenye iftar iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), MwanaFA alisema Watanzania wakiongozwa na mwana-Michezo namba moja nchini Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, watakuwa nyuma yao hivyo wakatangulize uzalendo, maarifa na mbinu ili kushinda mchezo huo.
Alisema licha ya kwamba, Stars wanakwenda kucheza na timu namba moja Africa, Taifa Stars wana uwezo wa kushinda mchezo huo ikiwa watajituma na kuwa na dhamira ya dhati, uzalendo wa nchi, wanaweza kushinda mchezo huo.
Alisema mchezo huo ni muhimu kushinda kutokana na kwamba ushindi utaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kufudhu kucheza kombe la Dunia mwakani.
"Morocco watakuwa wachezaji 11 na sisi tutakuwa 11 mkiweka dhamira na uzalendo ari bidii kwa maelekezo ya kocha wenu mtashinda, mmecheza Michezo mingi migumu kabla mkashinda na mnaweza kufanya hivyo tena Morocco," alisema Naibu Waziri huyo.
Alisema serikali inatambua umuhimu wa Michezo na ndiyo maana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akijitoa kuhakikisha anatenga fedha za kusaidia Michezo.
"Tunamshukuru Rais kwa jitihada zake binafsi, serikali kwa kujitoa katika michezo pamoja na mahitaji mengine ya nchi lakini anaunga mkono kutoa fedha kwa vilabu na Timu ya Taifa, " alisema.
Kuhusu shirikisho la Mpira wa Miguu TFF, Naibu Waziri alimpongeza Rais Wallace Karia na timu yake kwa kufanya vizuri katika kipindi cha miaka minne kwa kuzifanya timu za Taifa mbalimbali zinashiriki mashindano ya CAF.
"Mnyonge Mnyonge, haki yake mpeni, mimi sitaki usemi huu...Hanyongwi mtu na haki yake atapewa," alisema na kuongeza kusema kuwa,.
"Karia na wenzake wanafanya mambo makubwa hata kuna rafiki yangu mmoja aliwahi kuwa kiongozi TFF aliniambia Hawa wenzetu sijui wanafanya vipi, wanaweza kuzifanya timu za Taifa kushiriki mashindano mbalimbali ya Afrika,".
Alisema katika miaka ya hivi karibuni shirikisho hilo limeiheshimisha Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi tatu ambazo zimeweza kuingiza timu saba katika mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Nchi nyingine ni Senegal na Morocco.
Alisema Tanzania katika miaka 39 haikuwa imeshiriki mashindano ya Afcon tangu mwaka 1980 waliposhiriki kwa mara ya kwanza kule nchini Nigeria lakini kupitia Rais Karia na wenzake wamefanya hivyo Sasa mara tatu katika miaka minne hii.
Alisema katika historia ya Tanzania hakuna uongozi wa soka nchini katika shirikishi hilo ambao wameweza kufanya hivyo na kwamba serikali inaipongeza shirikisho hilo kwa kazi nzuri inayofanya.
"Hongereni akina Karia na wenzako akina Nyamlani (Athumani Makamo wake,) Kidau (Wilfred Katibu Mkuu TFF) najua wanakusaidia kufanya mambo yaende vizuri," alisema.
Pia alimpongeza kocha Hemed Morocco kwa kuchagua kikosi bora cha Timu hiyo ambayo hata watu wasiokuwa na elimu ya ukocha wameshindwa kukosoa wachezaji walioitwa kwakuwa kocha huyo amegusa na kudhingatia kila eneo la uchezaju na kuchagua kikosi bora ambacho hapan'shaka kitatuwakilisha vema.
Awali Rais wa TFF Karia alisema kuwa Stars itaondoka Ijumaa kuelekea Morocco kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) na kuwataka Watanzania kuiombea timu hiyo ambayo ikishinda itakuwa imetanguliza mguu mmoja wa kufudhu kombe la Dunia.











.jpg)






Comments
Post a Comment