Hakuna Taifa Lisilokopa Duniani, Uchumi wa Dunia Umejengeka Kwa Mikopo. Kukopesheka ni Ishara ya Uchumi Imara
_Deni la Tanzania ni himilivu na lina afya kiuchumi ukilinganisha na Mataifa mengi ya Afrika na ulimwenguni._
Na Bwanku M Bwanku.
Kwa siku za hivi karibuni kwenye Taifa letu kumezuka mjadala kuhusu nchi kukopa ama kutokukopa. Je kuna haja ya kukopa au kutokukopa au lipi ni lipi? Kama mwananchi nami ningependa kutoa mchango wangu kwa faida ya wote kuhusu huu mjadala.
Je ni muhimu kukopa? Hatuwezi kuleta maendeleo yetu wenyewe bila kukopa? Na maeneo mengine kama hayo yanayozunguka kwenye mjadala huu.
Kwa Mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyosomwa Wiki iliyopita Alhamisi Machi 27, 2025 Deni la Taifa hadi kufikia muda huu ni Trilioni 97. Deni hili linahusisha mikopo kutoka kwenye Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi n.k ambazo fedha zote hizo zikikopwa zinaelekezwa kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya Taifa.
Kwanza, ni muhumu ikafahamika kwamba hakuna nchi yoyote duniani inayofanya shughuli za kiuchumi kutekeleza miradi ya maendeleo bila kukopa. Hata nchi tajiri ulimwenguni zinakopa kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na miradi mbalimbali ya maendeleo tena zenyewe zikiwa na madeni makubwa sana kwenye Taasisi za Kimataifa za Fedha, Mabenki, Sekta binafsi n.k.
Mpaka sasa Deni lote la Dunia ni zaidi ya Dola za Marekani Trilioni 315 yani mara 3 ya uchumi wa Dunia nzima ambao ni takribani Dola za Marekani Trilioni 105.
Kwa Mujibu wa Takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Mataifa makubwa pamoja na yale yanayokua kwa kasi kiuchumi kama Marekani, China, Vietnam, Japan, India na mengine mengi ndiyo yanaongoza kuwa na mikopo mikubwa. Zaidi ya asilimia 60 ya madeni yote ya Dunia yanadaiwa na Mataifa haya makubwa na yale yanayoendelea kwa kasi.
Kwenye uchumi huu wa Dunia ya kisasa na shindani, hakuna nchi inaweza kufanya maendeleo yake bila kukopa au kushirikiana na Sekta binafsi kupitia Public-Private Partnership (PPP). Haipo Serikali inaweza kufanya mambo yote yenyewe bila kushirikiana na kutumia hizo PPP kwa kukopa kwenye Mabenki, Taasisi za Kifedha na hizo Sekta binafsi.
Na sio kukopa tu bali kuruhusu pia sekta binafsi kuingia kwenye mzunguko wa uchumi na utoaji huduma kwa watu na serikali kukusanya kodi yake tu, kitu ambacho sasa kinafanyika duniani kote.
Na hata katika hesabu ya kawaida tu, uwezo wa kukopeshwa unaendana na uimara wa uchumi. Hayupo mtu anaweza kukukopesha kama hauko imara. Kwa Taifa, uchumi imara unaozalisha, unaosafirisha bidhaa nje, uchumi madhubuti ni kigezo cha kukopesheka kama ambavyo Taifa letu lilivyo imara ndiyo maana linakopesheka. Huwezi kukopesha kitu kisichoeleweka
Hiyo ndiyo kanuni ya uchumi, serikali haiwezi kufanya kila kitu yenyewe.
IMF wametoa afya ya deni na uchumi wa Taifa ambapo Tanzania bado iko wastani wa chini wa asilimia 47 kutoka wastani usiotakiwa kuvuka asilimia 65. Mataifa majirani na mengi ya Afrika yamevuka wastani wa afya wa Deni la Taifa kwa uchumi wa Nchi. Mfano Kenya wako asilimia 70, Rwanda 71, Uganda 51, Msumbiji 96, Malawi 84, Namibia 67, Congo 70.
Tanzania bado iko mbali na mstari wa hatari wa Deni kuwa kubwa na bado inaendelea kuwa na uhimilivu wa deni kwa wastani wa chini kwa asilimia 47 ukilinganisha na Mataifa ya wenzetu ambayo yamevuka hadi mstari wa hatari wa Deni.
Kwa Takwimu za IMF na zile za Global debt, Marekani, Ulaya, China na Japan ndizo nchi zinazoongoza kwa kukopa ulimwengu. Marekani pekee yake inashare asilimia 31.8 ya Deni lote la Dunia kwenye Mashirika ya Fedha Duniani na Taasisi zake za Sekta Binafsi. Japan anashare asilimia 18.8 ya Deni lote la Dunia, wakati China yuko zaidi ya asilimia 10 na Ulaya ikiongozwa na Uingereza iko pia zaidi ya 10%.
Afrika nzima kwenye Deni zima la Dunia iko chini ya asilimia 2 wakati Mataifa Makubwa kuanzia Marekani, Japan, China na Ulaya yako zaidi ya asilimia 60 ya Deni zima la Dunia kwenye hizi Taasisi za Fedha (IMF na WB) na nyinginezo.
Kwahiyo haipo nchi isiyokopa Duniani, mjadala ni unakopa kupeleka huo mkopo wapi? Kama unakopa unakwenda kulipa mishahara na kufanyia shughuli zingine za anasa, hapo ndipo unaweza kuhoji ubovu wa kukopa lakini kama unakopa kujenga Reli za kisasa, huduma za wananchi na vitu vya namna hiyo, hakuna ubaya hata kidogo kukopa kwenye calculation za uchumi kwasababu unakopa, unawekeza halafu uwekezaji wako unapoanza kulipa unakuwa unalipa mkopo wako kidogokidogo huku ukiwa umeshaimarisha huduma, kutoa ajira kwa watu wako, kuzungusha uchumi n.k.
Muhimu mikopo hiyo ni kudhibitiwa ipasavyo na kuhakikisha inatumika ipasavyo kwenye shughuli tarajiwa za maendeleo na uchumi.
Kinachoangaliwa kwenye kukopa ni unakopa kwa ajili ya nini? riba ikoje. Kwa mfano Mikopo yote tunayokopa Tanzania ina riba ndogo sana na yote inakwenda kwenye shughuli za kiuchumi na uzalishaji. Yako Mataifa ya wenzetu majirani nisingependa kuyataja tunasikia yanakopa kwa ajili ya kulipa mishahara, riba yake kubwa na mikopo ya muda mfupi. Kwenye calculation za uchumi aina hii ya ukopaji ndiyo inakatazwa na ni mbaya sana.
Lakini Taifa letu mikopo yote inayochukua hakuna inayokwenda kwenye matumizi ya kawaida na anasa, yote inakwenda kwenye shughuli za maendeleo hasa kugharamia miradi ya maendeleo ambayo itakuja kuchangamsha shughuli za maendeleo za wananchi na Taifa na hivyo kuinua uchumi na kupata maendeleo huku ukiwa unalipa kidogokidogo na wakati huo ushafanya tayali maendeleo yako.
Mfano, tumekopa kugharamia ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu, kufanyia maboresho makubwa kwenye sekta ya afya na kadhalika.
Hii yote itainua uchumi wa mtu mmoja mmoja huku tukilipa kidogokidogo. Hata mkopo ule mkubwa kutoka Korea Kusini wa Trilioni 6.7 ni nafuu sana na riba yake ni ndogo mno ya asilimia 0.01 huku ukianza kulipwa baada ya miaka 25 ijayo.
Hayupo Tajiri au nchi Tajiri inatekeleza miradi yake mikubwa na ya kimkakati kwa kutumia tu fedha zake za walipa kodi, haipo nchi ya namna hiyo Duniani. Lazima ushirikiane moja kwa moja au nusu na Sekta binafsi kujenga uchumi wako.
Matajiri wote na Mataifa yote Matajiri yanaingia Ubia na Makampuni makubwa na Taasisi za Kifedha wanapata mkopo halafu wanatekeleza uwekezaji wake halafu baada ya kumaliza na mradi ukianza kutoa matokeo na kuanza kazi, unakuwa unarejesha kidogokidogo kwa masharti na makubaliano mliyojiwekea. Hiyo ndiyo kanuni ya uchumi inayocontrol na kuendesha uchumi kote ulimwenguni.
Kwahiyo kwenye mikopo hii unachoweza kujadili labda ni mikopo hii iwe ya kulipwa kwa muda mrefu, isiwe na riba kubwa, isiwe ya kibiashara na fedha zote za mikopo ziende kwenye shughuli za maendeleo na mzunguko wa kiuchumi, jambo ambalo mikopo yote ambayo tunaikopa hapa Tanzania kwenye Taasisi hizi za Kifedha inaingia kwenye maeneo niliyoyataja.
Ndio maana unasikia Marekani inauza Treasury Bonds zake na nchi kama China inazinunua za thamani hadi dola za kimarekani Trilioni 1, huko ndio kukopa kwenyewe ili watekeleze miradi ya maendeleo.
Na huu mjadala wa kukopa ndiyo hiyo sababu inatufanya hadi leo Afrika tunakabiliwa na changamoto za kutokuwa na barabara za kutosha, hatuna reli za kutosha, hatuna maji ya kutosha, hatuna vituo vya afya vya kutosha, hatuna madarasa ya kutosha n.k
Wakati nchi za Afrika hazikopi vya kutosha ili kuweka hiyo miundombinu ya msingi, nchi tajiri zilizoendelea wanakopa ku-upgrade miundombinu ambayo tayari wanayo ili wapate maendeleo zaidi. Mfano hivi sasa China wanayo reli ambayo treni inasafiri kwa spidi ya km 300 kwa saa, sasa wamekopa kujenga reli yenye spidi ya kilomita 600 kwa saa. Sasa kuna kosa gani sisi kukopa kujenga barabara? Kama Nchi tajiri zinakopa kuvumbua teknolojia itakayofanya uzalishaji viwandani ufanywe na robot badala ya binadamu, kuna kosa gani sisi kukopa kwa ajili kujenga madarasa yatakayosaidia watoto wetu wasome kwa staha?
Kama wenzetu wanakopa kwa ajili ya kwenda mwezini, kuna ubaya gani sisi kukopa kujenga reli ya Kaliua-Mpanda-Kalema? Kuna ubaya gani kukopa kupeleka Reli Dodoma, Tabora, Mwanza na kuendelea ambayo itafanya nchi yetu kuwa kitovu cha uchumi wa Afrika Mashariki kwa kusafirisha mizigo na nchi yetu kupata mapato makubwa sana yatakayotuwezesha kulipa kidogokidogo hiyo mikopo huku tukirahisisha sana shughuli zetu za kiuchumi na kijamii kwa miundombinu mizuri ya haraka.
Hivyo ni muhimu sana kuielewa dhana ya nchi kukopa sio jambo geni na wala sio jambo baya na kila nchi duniani inakopa. Serikali inavyokopa kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo inapaswa kuungwa mkono na sio kubezwa. Jambo la msingi ni lile alilosema Mhe Rais Samia kwamba tunapokopa miradi itekelezwe kwa ufanisi na kuzingatia thamani ya fedha inayotumika kutelekeza mradi "value for money".
Lakini pia tunakopa kupeleka kwenye shughuli za ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi kama ujenzi huo wa reli na mengine ya maendeleo ambayo yanatuhakikishia kuimarisha zaidi uchumi wetu, mapato na kurahisisha shughuli za watu na maendeleo huku tukilipa polepole. Hiyo ndiyo kanuni ya uchumi inayoendesha Dunia na inayotumiwa na nchi matajiri wote Duniani.
Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na Bwanku M Bwanku ambaye ni Afisa Tarafa wa Tarafa ya Katerero iliyoko mkoani Kagera.

Comments
Post a Comment