Chama cha Demokrasia na Maendeleo leo, Jumanne Machi 18.2025 kimemueleza Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusiana na msimamo wake wa 'No Reform, No Election' unaolenga kushinikiza mageuzi makubwa ya mifumo ya uchaguzi nchini, na kwamba endapo mageuzi hayo hayatafanyika basi chama hicho kupitia 'nguvu ya umma' kimejipanga kuzuia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu
Akizungumza na wanahabari nje ya viunga vya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa muda mfupi baada ya kutoka kwenye ofisi hizo, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika amesema viongozi wa chama hicho wamelazimika kufika kwenye ofisi hizo kufuatia wito walioupokea hivi karibuni ambao pamoja na mambo mengine uliwataka kufika hapo ili kueleza wanamaanisha nini wanaposema 'No Reform, No Election'
Kupitia kikao hicho kilichochukua zaidi ya saa nne, Mnyika amesema viongozi wa CHADEMA wameieleza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa kauli hiyo hawajaitoa kwa bahati mbaya kwani kwa muda mrefu nchini kumeshuhudiwa chaguzi ambazo zisizokuwa huru na haki zisizoheshimu maoni ya wananchi wanayotoa kupitia masanduku ya kura, na kwamba mara zote imeelezwa na wadau mbalimbali kuwa mwarobaini wa yote hayo kufanyika kwa mageuzi ya mifumo ya uchaguzi ikiwemo kupatikana na Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, jambo ambalo linaonekana kupigwa chenga na watawala (Serikali na CCM)
"Sisi (CHADEMA) tunaamini baada ya kutuita na sisi kuitikia wito wao, sasa wanapaswa kuyachukulia kwa uzito ili na wao (Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa) wawe na mchango kama wadau wengine tuliokutananao, mchango wa kuwezesha kufanyika kwa mageuzi na mabadiliko kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025, bila mabadiliko hakuna uchaguzi (No Reform, No Election) tunaamini jambo hili linapaswa kukubalika na wadau wote" -Mnyika
Hata hivyo, Mnyika amesema taasisi hizo mbili (CHADEMA na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa) baada ya kikao hicho wanatarajia kukutana tena hivi karibuni kwa mazungumzo mengine, lakini wakati hayo yakiendelea chama hicho kimeendelea kusisitiza msimamo wake uko palepale na hautabadilika na kwamba hivi karibuni wataanza kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ya nchini kuwaeleza wananchi kuhusiana na hilo ikiwemo kufanya vikao na mikutano ya hadhara
Alipoulizwa kuhusu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuendesha zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la mpiga kura, Katibu Mkuu huyo amebainisha wao kama chama walishatoa msimamo wao tangu Desemba 2024 walipoombwa kutoa maoni kuhusu kanuni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, ambapo kupitia barua yao waliyoituma kwa INEC walieleza wazi kuwa hawawezi kutoa maoni kuhusu kanuni hizo pasipo kufanyika kwa marekebisho yatakayowezesha uwepo wa chaguzi huru na haki
"Kwa hiyo katika hatua hii niwaombe tu vyombo vya habari badala ya kutuuliza kuhusu 'Tume' na yanayoendelea ya uandikishaji, kawaulizeni 'Tume ya Taifa ya Uchaguzi' ni kwa nini tangu mwezi Desemba hadi sasa hawajajibu barua yetu tuliyowaandikia ya kupata reform, sisi tumeshaweka msimamo bayana kwamba tunachokitaka kwa sasa ni mabadiliko ya Kikatiba na kisheria ya kuwezesha uchaguzi huru na haki kabla ya hatua nyingine zozote zinazohusiana na uchaguzi na tunataka wadau wengine wote watuelewe kwenye hili" -Mnyika
Katika kikao hicho, Mnyika aliambatana na Naibu Katibu Mkuu Bara Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Wakili Ally Ibrahim, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Dkt. Rugemeleza Nshala, na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Brenda Rupia.


.jpg)



Comments
Post a Comment