📍Serikali yasema itaenzi kazi zake
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA, ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Balozi Juma Mwapachu aliyezikwa leo Machi 30 Kijijini kwao Pande Jijini Tanga.
Katika mazishi hayo yaliyoongozwa na Jaji Mstafu wa Mahakama Kuu Jaji Osman Chande, MwanaFA alisema kuwa serikali imempoteza mtumishi bora hivyo itahuisha yale yote mema aliyoyaacha wakati wa utumishi wake.
Alisema marehemu wakati wa uhai wake alikuwa mchapakazi aliyefanya kazi kwa maslahi Mapana ya nchi yake, uzalendo lakini pia alikuwa mwaminifu aliyeongoza wenzake vizuri.
"Kiukweli tumepoteza mtu muhimu, mtu makini mchapa kazi aliyejali nchi yake na aliyeongoza wenzake katika njia sahihi, alisema.
MwanaFA ambaye ni mbunge wa Muheza alisema kwa niaba ya serikali wataenzi yote aliyoasisi marehemu katika ngazi mbalimbali za utumishi alizopitia ikiwemo nafasi aliyostafu nayo ya Katibu Mkuu wa EAC.
Jajj Mstaafu Chande Othman akiongoza waombolezaji waliojitokeza kumzika marehemu, aliwataka watumishi nchini kuiga uzalendo aliokuwa nao wa nchi yake.
Alisema Balozi Mwapachu alikuwa mbunifu wa kuiunganisha Afrika Mashariki anayestahili kuigwa na kuhuisha yale yote aliyoyaasisi.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba alimwelezea Mwapachu kama ni baba aliyemlea na kumpa miongozo mingi ya namna bora ya kuitumikia nchi na Serikali kwa ujumla.
"Mzee Mwapachu amenilea na kuniongoza kwa mambo mengi juu ya namna bora ya kuitumikia nchi na Serikali kwa ujumla.... tumempoteza kiongozi bora na mzalendo wa dhati kwa nchi yake" alisema Makamba.
Sala ya mazishi katika makaburi ya ukoo wa Mwapachu yaliyopo katika Mtaa wa Pande Jijini Tanga, yaliongozwa na Sheikh Mohamed Idd.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Kiongozi Mkuu mstaafu wa Chama Cha ACT Wazalendo Zito Kabwe, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba, mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali na watumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Marehemu nyumbanii kwake Chumbageni Jijini Tanga, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na msaidizi wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dkt Abdul Makame alisema Mwapachu ni Katibu Mkuu wa tatu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini kazi zilizofanywa katika kipindi chake zimekuwa mwongozo hadi sasa.
"Pamoja na kwamba Mwapachu alikuwa Katibu Mkuu wa tatu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini hadi sasa miongozo aliyoiacha imekuwa rejea Kwa masuala mengi ya kiutendaji ya Jumuiya yetu"alisema Dkt Makame.




Comments
Post a Comment