Na Angela Sebastian ;Bukoba
VIONGOZI wa madhehebu yote mkoani Kagera wamewataka wananchi wa mkoa huo kutambua kuwa hakuna utajiri na mafanikio yanayopatikana kupitia njia za kishirikiana au kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Pia wamekemea baadhi ya wananchi wa mkoa huo ambao uendekeza fitina mioyoni mwao maarufu kama kamunobele ambayo imekuwa jinamizi linaloendelea kuwatesa baadhi ya wananchi mkoani humo na kusababisha kutojifanyia maendeleo na kujiingizia kipato.
Viongozi hao walitoa kauli hizo jana wakati wa dua na maombezi ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan,wasaidizi wake,Taifa mkuu wa mkoa na wananchi kwa ujumla ambapo ilifanyika katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba.
Makamu askofu wa kanisa katoriki la Bukoba ambaye pia ni baba paroko wa parokia ya Bukoba padre Samueli Muchunguzi amesema katika kitabu cha Zaburi 127 sura ya kwanza inasema bwana asipojenga nyumba wajengaji wengine wanafanya kazi bure na asipolinda mji walindao wanakesha bure.
Amesema ndiyo maana viongozi na wananchi wa mkoa wa Kagera wameamua kuweka dua na maombezi ili kuomba kwa Mungu kumkabidhi kila wafanyayo kwa ajili ya maendeleo ya watu wao yawe wenye tija na wasikeshe bure.
Pia padre Muchunguzi akawaombea wananchi na viongozi wote kuishi katika uadilifu ,kutenda haki na kuondokana na jinamizi la fitina na wivu ambalo linasumbua wananchi wa mkoa huo na kusababisha baadhi yao kutoelewana na kujenga chuki zisizo na faida badala ya kujiletea maendeleo.
Aidha amemuomba Mungu abariki Taifa letu liendelee kuska amani na mataifa mengine hasa yale yanayopinga ushoga,usagaji, kubadili jinsia matumizi ya madawa ya kulevya na mambo yote yasiyofaa yanayohaibisha utu wetu.
Shekhe Abdushahidu Abbas kiongozi mkuu wa Answar Sunna Tanzania (JASUTA) ambaye ni mmoja wa viongozi walioshiriki katika dua na maombezi hayo ambapo alisema kuwa wananchi wanapaswa kutambua kuwa, utajiri na mafanikio haviwezi kuja kwa njia ya kuua watu na kuwakata viungo watu wenye ualbino bali huja kwa ushirikiano wa pamoja na kumtanguliza Mungu.
Abbas amesema pia wapo wanaodhani kupata nafasi za uongozi ni lazima utumie njia za kishirikina jambo ambalo si kweli bali wanapaswa kumtanguliza Mungu na kumuomba ili awezekukujalia kumudu nafasi hiyo.
Naye shekhe wa mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta aliombea uwepo wa upendo,uvumilivu na amani ya nchi yetu na kati ya wananchi na viongozi wao ili tuwezekujenga Taifa lenye ustawi linalopendeza na kuvutia ndani na nje ya nchi yetu.
Kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa amesema shughuli hiyo maalumu ya dua na maombezi ni tukio linalofungua shughuli ya Tamasha kubwa la Ijuka Omuka la 2024 ambalo limeasisiwa na mkuu huyo wa mkoa lenye lengo la kuonyesha fulsa mbalimbali zinazopatikana mkoani humo kwa kuwashirikisha wazawa wa mkoa huo na wadau mbalimbali walioko ndani na nje ya mkoa na nchi.
Ametaja madhehebu yaliyoshiriki katika dua na maombezi kuwa ni Tec,Cct,Shia,Bakwata,umoja wa makanisa ya kipentekoste na Jasuta.
Tamasha hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Naibu waziri mkuuu na waziri wa Nishati Doto Biteko Desemba 19 mjini na litamalizika Desemba 26 mwaka huu.