Waziri Kombo;Tanzania itaendelea Kuunga Mkono Juhudi za Kuleta amani na Usalama Ukanda wa Maziwa Makuu
Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameeleza kuwa Tanzania ikiwa ni mwasisi wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Mkuu (ICGLR) itaendelea kushirikiana na nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo na Jumuiya ya Kimataifa katika juhudi za kutafuta amani ya kudumu kwenye ukanda huo.
Waziri Kombo ameeleza hayo alipozungumza katika Mkutano wa Kawaida wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi Wanachama wa ICGLR uliofanyika jijini Luanda, Angola tarehe 24 Novemba 2024.
Akizungumzia kuhusu msimamo, mchango na nafasi ya Tanzania katika kufatua amani na usalama kwenye ukanda wa Maziwa Makuu Waziri Kombo ameeleza kuwa, Tanzania chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itafanya kazi bila kuchoka kwa kushirikiana na nchi wanachama na Jumuiya ya Kimataifa kutatua migogoro iliyopo ili kuwa na ukanda wenye amani, ustawi na ustahimilivu.
“Kama mwanachama mwanzilishi wa ICGLR, Tanzania inaamini kuwa kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia na kuimarishwa kwa utulivu kutaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi ya watu wetu katika Ukanda wa Maziwa Makuu” Ameeleza Waziri Kombo.
Aidha, Waziri Kombo licha ya kueleza utayari wa Tanzania katika kuendelea kushirikiana na wadau katika kurejesha amani na usalama kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, ametoa wito kwa nchi wanachama kuhakikisha kuwa ushawishi wa washirika wa maendeleo hauathiri utendaji na ufanisi wa mifumo iliyowekwa ikiwemo Mfumo wa Tahadhari ya Mapema na Majibu ya Migogoro wa ICGLR (ICGLR Conflict Early Warning and Response Systems).
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa nchi Wanachama kuheshimu na kutimiza wajibu wake wa kuchangia fedha kwa Sekretarieti, ikiwa ni ishara ya mshikamano na juhudi za pamoja, katika kuhakisha Jumuiya inatekeleza mipango na mikakati inayojiwekea ili kufikia matarajio ya kuwa na ukuanda wenye Usalama, Utulivu, na Maendeleo endelevu.
Pia ametumia fursa hiyo kuitaka Sekretareti ya ICGLR kuzingatia matumizi mazuri na usimamizi mzuri wa fedha kwa manufaa ya kanda.





Comments
Post a Comment