Mkuu wa jeshi la kujenga Taifa (JKT) meja Jenerali Rajab Mabele ameongoza maafisa,askari na mamia ya wananchi katika mazishi ya mmoja ya wasaidizi wake meja Ayub Ally Pazi aliyefariki kwa ajali ya gari Novemba 9 mwaka 2024 katika maeneo ya Nanenane mjini Dodoma.
Akitoa neno la pole kwa mamia ya waombolezaji nyumbani kwa wazazi wa wa marehemu Kiwalani jijini Dar es salam kabla ya kufanyika kwa mazishi hayo,mkuu huyo wa JKT amesema taarifa za kifo cha meja Pazi alizipokea kwa mshtuko mkubwa.
"Siku ya ijumaa tarehe 8 mwaka 2024 alikuja nyumbani kuniletea nyaraka ili nizifanyie kazi kabla ya jumatatu,ilipofika jumamosi tarehe 9 niliambiwa kuna ajali imetokea eneo la Nanenane na Meja Pazi amefariki!
Kwa kweli taarifa zile nilizipokea kwa mshutuko mkubwa hasa ukizingatia tulikua nae jana yake na jinsi alivyokuwa karibu nami kama msaidizi wangu"alizungumza Meja Jenerali Mabele kwa masikitiko makubwa.
"Mimi nilimkuta ofisini alikuwa msaidizi wa mtangulizi wangu,nami niliendelea nae, kwa vile mimi nilikuwa mgeni katika hii ofisi meja Pazi alinisaidia sana kwa mambo mengi...kuna wakati kazi nyingi alizifanya yeye, kwangu alileta kwa baraka tu ili mimi niseme ndio au hapana,hivyo tumepoteza kijana mchapa kazi na msikivu na jeshi pia limepoteza mtu muhimu,alitumia elimu na taaluma yake kwa ajili ya kulisaidia taifa lake" alisema meja Jenerali Mabele
Amesema kuwa kwa vile sisi sote ni binadam na yeye ametangulia ni vema tukubali na kikubwa kwetu kuendelea kumwombea kwa mwenyezi Mungu
"Nitaendelea kumkumbuka sana hasa nitakapokutana na baadhi nyaraka zake ofisini ambazo zimeandikwa kwa mkono wake"alisema meja Jenerali Mabele huku akionesha kuumizwa mno na kifo cha afisa huyo.
Mwakilishi wa mkuu wa majeshi katika mazishi hayo brigedia Jenerali Chuli,amesema mkuu wa majeshi amesikitishwa na kifo na afisa huyo na kutoa pole kwa mkuu wa jeshi la kujenga Taifa,maafisa na askari pamoja na familia ya marehemu na kuwaomba kuwa na moyo wa subra katika kipindi hiki kigumu.
Mmoja ya kiongozi wa dini ya kiislam akizungumza mbele ya waombolezaji amesema mbali na jeshi kupoteza nguvu kazi jamii hiyo imepatwa na mshutuko mkubwa kufuatia kifo hicho ambacho kimesababisha majozi kwa kila mmoja katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa wasifu wa marehemu,meja Pazi ambaye amezikwa katika kidini na kwa heshima zote za kijeshi katika makaburi ya Kibamba Msakuzi ameacha mjane na watoto.










