Waziri Kombo ahimiza ushirikiano wa nchi Marafiki ujikite katika biashara

GEORGE MARATO TV
0


Tanzania imesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na nchi marafiki, ikiamini kuwa hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 09, 2024 jijini Helsinki, Finland na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati anashiriki kikao cha Mashauriano ya Kisiasa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Elina Valtonen na Naibu Mawaziri wa Wizara hiyo, Mhe. Pasi Hellman anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Kimataifa na Mhe. Jarno Syrjälä anayeshughulikia Biashara za Kimataifa.

Waziri Kombo amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mabadiliko makubwa ya mifumo ya sera na sheria ili kuboresha mazingira ya biashara kwa lengo la kuvutia uwekezaji nchini Tanzania. Hivyo, ametoa wito kwa wawekezaji wenye mitaji na dhamira ya dhati ya kuwekeza, waondoe hofu kuhusu Tanzania, kwani nchi hiyo ni mahali salama kwa wawekezaji na mitaji yao.

Waziri Kombo ameishukuru Serikali ya Finland kwa kufanya juhudi kubwa ya kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali kama vile misitu, TEHAMA, mifumo ya ulipaji kodi, hali ya hewa na elimu. Alisema juhudi hizo zimechangia kuifikisha Tanzania hapa ilipo na kuwaomba mawaziri hao waendeleze juhudi hizo, huku wakihimiza kampuni za nchi yao kuja kuwekeza Tanzania ambayo ina fursa nyingi hazijaweza kutumiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji midogo na teknolojia duni.

Maeneo ambayo Balozi Kombo ameyainisha kwa Finland kuyapa kipaumbele katika ushirikiano wake na Tanzania ni pamoja na uhawilishaji wa teknolojia (technology transfer), nishati, viwanda vya kuongoza thamani, elimu ya ufundi, masuala ya kijinsia na haki za wanawake na masuala ya kidijiti.

Amesema maeneo hayo yakifanyiwa kazi ipasavyo, yataongeza nafasi za kazi na ni suluhisho la moja kwa moja la tatizo la ajira nchini.

Mhe. Kombo aliendelea kwa kusema kuwa ni wakati muafaka wa nchi ya Finland kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana wa Tanzania katika fani ambazo nchi hiyo pia inazihitaji kwa kiasi kikubwa.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top