Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) imefanikiwa kukuza ufaulu na kupunguza Sifuri katika Mkoa wa Kusini Unguja kwa Asilimia 84 Mwaka 2022/2023 kutoka Asilimia 68 kwa Mwaka 2020/2021.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mhe.Wanu Hafidh Ameir amebainisha hayo visiwani Zanzibar wakati wa maadhimisho ya siku ya saratani.
Mhe.Wanu ameongeza kuwa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) pia inajivunia kuweza kuwasomesha Wanafunzi 114 walioshindwa kuendelea na Elimu ya Juu mafunzo ya Amali takribani Wanafunzi 114 katika Vyuo vya Amali ikiwemo Makunduchi na Mkokoteni.
"Katika suala la Afya, Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) tumekuwa tukishajihisha Vijana, Wanawake na Wanaume kwenye Afya ya Akili kupitia Semina mbalimbali na Michezo kama vile Marathon, Netball, Football na Michezo mingine mbalimbali" Alisema Mhe. Wanu Hafidh Ameir na kuongeza kuwa
"MIF kwenye masuala ya Afya, tumeweza kuwabadilisha akina Mama takribani 2,000 kutoka kwenye matumizi ya Nishati Chafu ikiwemo uni na Mkaa na kuwapeleka katika matumizi ya Nishati safi na salama ya kupikia kwa kuwapatia mitungi ya gesi. Hii ni kuunga mkono jitihada za Serikali zetu mbili"
Mhe.Wanu amesema lengo la MIF kubeba Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ni kuwakinga akinamama kutokana na madhara ya kutumia Kuni na Mkaa ambapo hupata athari kutokana na moshi wakati wa kupika.
Katika kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani, Mwenyekiti wa Taasisi ya MIF Mhe.Wanu Hafidh Ameir amesema kuwa Taasisi hiyo ikishirikiana na Taasisi ya Huduma ya Afya Aga Khan na Wizara ya Afya Zanzibar imeandaa siku mbili Maalum ya maadhimisho kwa kuipa kipaumbele jamii kupata elimu juu ya Saratani ya Matiti na Saratani ya Nyonga ya Kizazi na Tezi Dume kwa upande wa akina Baba na kufanya uchunguzi wa awali wa Saratani hizo.
"Nichukue nafasi hii niwaombe wale wote waliofika hapa wasikose kupima Saratani hizi kwasababu hivi sasa imeshakuwa nyingi miongoni mwetu na hamna namna, inabidi na ni lazima tupime, nawaomba sana hasa akina Mama" - Mhe. Wanu
Ameeleza kuwa Tafiti zinaonyesha ugunduzi wa awali wa Saratani huokoa maisha kwa asilimia kubwa sana na kuwahimiza wananchi kujijengea utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara na pindi wanapoona au kuhisi viashiria waende kituo cha Afya kwa uchunguzi zaidi.
"Kupata elimu ni jambo moja lakini jambo la muhimu sana ni kupima ili kujua Afya yako. Nasisitiza tena hasa akina Mama kwa sababu mara nyingi sana ndiyo waathirika wakubwa wa maradhi ya Saratani" Amesisitiza Mhe. Wanu na kuongeza kuwa
"Inawezekana umeanza Kupata dalili za mapema za Saratani lakini hujui kuwa ndiyo dalili zenyewe. Moja ya dalili kwa akina Mama tukiwa kwenye siku zetu tunatokwa na damu sana. Tuna mtindo wa kusema mke mwenza kaniroga, Hapana!"
Aidha Mhe. Wanu ametoa Shukrani za dhati kwa Wizara ya Afya Zanzibar,Taasisi ya Afya Aga Khan na Wananchi kwa kujitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya Saratani na Uongozi wa MIF kwa kufanya maandalizi mazuri yaliyofanikisha maadhimisho ya siku ya saratani.
Pia amesisitiza dhamira ya Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) ya kuendelea kuunga mkono Serikali zote mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya Elimu, Afya na Uchumi.