Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema ili kufikia lengo la uchumi Jumuishi unaokuwa kwa kasi,unaoimarisha ustawi wa watu kwa kuboresha huduma za Jamii na kupunguza umaskini wa kipato,nchi inapaswa kuwa na mfumo mzuri wa ulipaji na ukusanyaji wa kodi.
Dkt.Samia ameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tume ya Rais ya kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi iliyofanyika ikulu ya chamwino.
Dkt.Samia amesema kuwa Tume hiyo imeundwa kwa lengo la kufanya tathmini ya mfumo mzima wa kodi,kuimarisha zaidi mfumo huo na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kurahisisha usimamizi wa kodi nchini.
"Licha ya uchumi wa nchi kukua kwa kasi,idadi ya watu kuongezeka na mahitaji ya huduma za Jamii na miundombinu kukua,bado asilimia 60 ya uchumi wa nchi unatokana na sekta isiyo rasmi" alisema Rais Samia na kuongezeka kuwa
"Serikali imedhamiria kujenga mfumo wa kodi unaotenda haki na utakaomuwezesha kila anayestahili kulipa kodi,kulipa kodi stahiki na kutoza kodi zote kwa mujibu wa sheria.
Pia Rais amesisitiza umuhimu wa nchi kuwa na mfumo wa kodi unaochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuchangia ujenzi wa uchumi Jumuishi unaoiwezesha serikali kuwa na vyanzo vya uhakika na vinavyotabirika ili kuleta ustawi kwa wananchi.