![]() |
Na Shomari Binda-Tarime |
WANANCHI wa Kitongoji cha Sang'anga Kijiji na Kata ya Nyabisanga wilayani Tarime mkoa wa Mara wameshukuru kupata mradi wa Rais Samia wa kuchimbiwa visima vya maji na sasa wana uhakika wa kupata maji safi na Salama
Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo julai 11 kijijini hapo wamesema kuyaona magari ya kuchimba visima na kuanza kufanya kazi hiyo ni ishara ya kuondokana na adha ya maji waliyokuwa nayo kwa muda mrefu.
Wamesema wamekuwa wakiamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji na kushindwa kujiandaa na shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo hivyo mradi huo umekuwa mkombozi.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Ghati Marwa amesema wanamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa visima vya maji kwaajili ya kuwatua ndoo kichwani.
" Tunashukuru sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu wa kutuletea visima vya maji huku kijijini kwetu.
" Kwa namna kazi zinavyoendelea kufanyika hapa tuna uhakika wa kuanza kupata maji na kuondokana na adha tuliyopata kwa muda mrefu",amesema.
Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini ( RUWASA) mkoa wa Mara Tulinumpoki Mwakalukwa amesema kwa sasa shughuli ya uchimbaji wa visima unaendelea vizuri jimbo la Tatime vijijini.
Amesema tayari visima 2 kati ya 5 vinavyotakiwa kuchimbwa jimbo la Tarime vijijini vimeshachimbwa na sasa wanaedelea na cha 3
Mwakalukwa amesema wananchi wanatoa ushirikiano kwenye maeneo ya miradi na hawajapata kusikia kuna changamoto zozote na baada ya hapo watahamia Musoma vijijini.
Amesema kisima kinachochimbwa kwenye Kijiji hicho ni moja ya visima 900 vya Dkt.Samia vinavyochimbwa kila jimbo visima 5 Tanzania nzima yakiwemo majimbo ya mkoa wa Mara.
Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Tarime Mohamed Mtopa amesema licha ya mradi wa visima 5 kila jimbo wa Rais Dkt.Samia ipo miradi mingine iayoendelea ya kumtua ndoo mama kichwani.
Amesema miradi hiyo inaendelea vizuri na wananchi wilayani Tarime wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama.

Comments
Post a Comment