Na Shomari Binda-Musoma
UONGOZI wa timu ya Yanga tawi la Musoma umeelezea mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa kipindi kirefu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa tawi hilo Marehemu Adam Said Gunje.
Akimzungumzia kiongozi huyo wa zamani aliyeongoza tawi la Musoma na kiongozi wa mkoa wa Mara kwa zaidi ya miaka 30, Mwenyekiti wa sasa wa Yanga tawi la Musoma na mratibu wa mkoa wa Mara Ismail Massaro amesema moja ya jambo kubwa alilolifanya Gunje ni kuwaunganisha wana Yanga.
Amesema kwa kipindi chote cha uongozi wake amekuwa karibu na wanachama na mashabiki wa Yanga Musoma na mkoa wa Mara na kupelekea kuwa na nguvu.
Massaro amesema aliposhika nafasi hiyo alipewa ushirikiano wa karibu na Adam Gunje katika kuendelea kuwaunganisha wana Yanga.
Amesema ili kuendelea kuweka kumbukumbu zake vizuri kwenye tawi la Musoma wataendelea kuiga mazuri yote aliyofanya ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wana Yanga.
" Ametangulia mbele ya haki mzee wetu lakini sisi kama Yanga tawi la Musoma tutaendelea kuiga mazuri yake yote.
Niwaombe wana Yanga wote tushiriki kwenye msiba wa mzee wetu ikiwa ni pamoja na kushiriki maziko yaliyopangwa kufanyika julai 22", amesema
Katika hatua nyingine akizungumzia kuelekea tamasha la wiki ya mwananchi Massaro amesema julai 30 wana Yanga tawi la Musoma wataenda kuitembelea hospital ya manispaa ya Musoma kwa kufanya usafi na kutoa damu.
Amesema licha ya usafi na kutoa damu wanatarajia kutoa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa watakao kuwa kwenye hospital hiyo siku ya tukio.

Comments
Post a Comment