Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Pascal Maganga amesema, kuanzia Januari hadi Juni 2024 miradi 409 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.09 tayari imesajiliwa katika kituo hicho na kwamba inatarajiwa kutoa ajira 121,209 pindi itakapokamilika.
Maganga amesema hayo wakati TIC ilipotembelea kiwanda cha maziwa cha Kahama Fresh kilichopo Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani.
"Kwa mwaka 2023, miradi 526 ya uwekezaji ilisajiliwa TIC yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.72 ikitarajiwa kutoa ajira 137,010," amesema Maganga
Katika jitihada za kuhamasisha uwekezaji wa ndani, TIC inatembelea miradi mbalimbali na kutoa elimu kwenye mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Simiyu, Lindi, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Katavi, na inashirikiana na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa upande wa Unguja na Pemba.
Chanzo: TIC


Comments
Post a Comment