Mkurugenzi wa Kampuni ya Colmat Bw. Tanziru Mahamudu Mkakere amesema ameridhishwa na huduma ya usuluhishi iliyotolewa na Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria baada ya kufanikiwa kutatua mgogoro wa kibiashara uliokuwa baina yake na kampuni ya Sewa.
Akizungumza leo Julai 11,2026 katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria lililopo kwenye maonesho ya 50 ya kimataifa ya wafanyabiashara maarufu kama Sabasaba Bw. Mkakere amesema mgogoro huo ulitokana na malipo ya kazi ya upakaji rangi wa takribani magari 200, ambapo walikubaliana kulipwa shilingi 270,000 kwa kila gari. Kiasi cha mkataba kilikuwa takribani shilingi milioni 54, lakini alilipwa shilingi milioni 48 pekee na kubaki na deni la takribani shilingi milioni 6.
Amesema kutokana na kuchelewa kwa malipo, mgogoro uliwasukuma kufika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria kwa ajili ya usuluhishi. Amesema kupitia huduma hiyo waliweza kusikilizwa, kuelewana na hatimaye kufikia makubaliano ya jinsi deni lililobaki litakavyolipwa.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, fedha zilizobaki zitalipwa kwa awamu nne za kila mwisho wa mwezi hadi deni litakapokamilika.
Kwa upande wake mkandarasi mdogo Bw. Sahewa Mwamba Chando, amesema walichagua kutumia huduma za usuluhishi wa Wizara ya Katiba na Sheria ili kuepusha kufikishana mahakamani.
Ameeleza kuwa wamepokelewa vizuri na kusaidiwa kufikia suluhu iliyowaridhisha pande zote mbili, jambo lililowezesha kuendelea na mahusiano yao ya kibiashara kwa amani.




Comments
Post a Comment