Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, ameendelea kusisitiza utatuzi wa kero za wananchi kwa vitendo baada ya kufanya mkutano wa hadhara na wakazi wa Kijiji cha Suguti, Kata ya Suguti, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, ambapo alisikiliza changamoto mbalimbali na kutoa maelekezo ya utekelezaji wa haraka.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Julai 9, 2026, Mhe. Mtambi aliliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kuanza taratibu za kuanzisha kituo kidogo cha polisi katika eneo la Suguti, kufuatia ombi la wananchi waliobainisha kuwa uwepo wa kituo hicho utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa wakazi pamoja na mali zao.
"Wananchi wanahitaji huduma za usalama karibu yao. Jeshi la Polisi lifanye taratibu za kuanzisha kituo kidogo cha polisi katika eneo hili ili kuongeza ufanisi wa ulinzi na usalama," amesema Mhe. Mtambi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliunda kamati maalumu ya kuchunguza malalamiko ya uchafuzi wa mazingira katika Kitongoji cha Karusenyi, Kijiji cha Suguti.
Kamati hiyo itaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka, na imepewa siku saba kuwasilisha taarifa yenye mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto hiyo.
Mbali na maamuzi hayo, Mhe. Mtambi alipokea na kutatua kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi, zikiwemo zinazohusu huduma za jamii, miundombinu na maendeleo ya eneo hilo.
Amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushughulikia changamoto zao kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya na wataalamu wa sekta mbalimbali.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kuendeleza utaratibu wa kusikiliza wananchi moja kwa moja, akitangaza kuwa wiki ijayo atafanya ziara katika eneo la Bugwema kwa lengo la kukutana na wananchi, kusikiliza kero zao na kutoa maelekezo ya kuzitatua kwa wakati.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma kwa wananchi na kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka kupitia ushirikiano kati ya viongozi na jamii.








Comments
Post a Comment