Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) umeendelea kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia baada ya kutunukiwa tuzo ya kimataifa na kutambuliwa kuwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali Mtandao duniani katika Tuzo za World Summit on the Information Society (WSIS) Prizes 2026, zilizofanyika Julai 8, 2026 jijini Geneva, Uswisi.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, na Mratibu Mkuu wa Tuzo za WSIS, Bi. Gitanjali Sah, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU).
Kwa mujibu wa ITU, NeST ilishinda katika kategoria ya Serikali Mtandao (e-Government), iliyoshirikisha zaidi ya mifumo 1,500 kutoka nchi 122 duniani. Mifumo hiyo ilitathminiwa kwa mchango wake katika kuimarisha uchumi shirikishi, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu kupitia matumizi ya teknolojia.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bw. Dennis Simba amesema mafanikio hayo yametokana na maono na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusukuma mbele ajenda ya matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma za umma.
"Tuzo hii ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na maono yake ya kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma," amesema Bw. Simba.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo pia yametokana na ushirikiano wa wadau wa sekta ya ununuzi wa umma walioendelea kuupokea na kuutumia mfumo huo kwa ufanisi, huku maoni yao yakichangia kuendelea kuuboresha.
Amebainisha kuwa NeST ni mfumo uliobuniwa na wataalamu wa Kitanzania, jambo linaloonesha uwezo wa ndani katika kubuni suluhisho za kidijitali zenye ushindani wa kimataifa.
Kwa sasa, michakato yote ya ununuzi wa umma nchini inafanyika kupitia Mfumo wa NeST, huku kufanya ununuzi nje ya mfumo huo kukiwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023.
Tuzo hiyo inaongeza hadhi ya Tanzania katika matumizi ya teknolojia za kidijitali serikalini na kudhihirisha hatua kubwa ambazo nchi imepiga katika kujenga mifumo yenye uwazi, uwajibikaji, ufanisi na thamani kwa fedha za umma.


Comments
Post a Comment