Na Angela Sebastian, Bukoba
Afisa Afya wa Mkoa wa Kagera, Yassin Mwinori, amewataka wakuu wa shule na walimu wakuu wa shule zote mkoani humo kuhakikisha wanafunzi wote wanaorejea shuleni kutoka likizo wanapimwa joto la mwili mara wanapowasili, ikiwa ni sehemu ya hatua za awali za kuzuia kuingia na kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola.
Mwinori ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akitoa elimu ya afya kwa wananchi katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ikiwemo zahanati, vituo vya afya na maeneo ya mipakani
Amesema licha ya ugonjwa wa Ebola kuripotiwa katika baadhi ya nchi jirani, Mkoa wa Kagera bado uko salama na hakuna kisa chochote kilichothibitishwa hadi sasa.
Amesisitiza kuwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu kati ya Tanzania na Uganda, hususan wanafunzi wanaovuka mpaka kwenda kusoma pande zote mbili, ni muhimu kwa shule kuchukua tahadhari za ziada ili kuzuia uwezekano wa maambukizi.
"Kwa sasa shule zimefunguliwa kuna watoto wa Tanzania wanaosoma Uganda na wa Uganda wanaosoma Tanzania hivyo, wanaweza kuvuka mpaka na kuingia shuleni bila kuonyesha dalili zozote za ugonjwa ni muhimu walimu wahakikishe wanafunzi wanapimwa kabla ya kuchangamana na wenzao ili tuendelee kubaki salama," amesema Mwinori.
Amefafanua kuwa mtu aliyeambukizwa Ebola anaweza kuwa hajaanza kuonyesha dalili wakati anavuka mpaka, lakini baadaye dalili zikajitokeza akiwa tayari shuleni, hali ambayo inaweza kuongeza hatari ya maambukizi kwa wengine iwapo tahadhari hazitachukuliwa mapema.
Mbali na hatua hizo, Mwinori amewahimiza wananchi kuendelea kuzingatia kanuni za usafi binafsi, ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, pamoja na kutoa taarifa kwa wahudumu wa afya wanapobaini mtu mwenye dalili zinazofanana na Ebola.
Aidha amesema tangu kutangazwa kwa mlipuko wa Ebola nchini Uganda mwezi Mei mwaka huu, Mkoa wa Kagera umesambaza mabango zaidi ya 17,000 katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huo, njia za maambukizi na hatua za kujikinga.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Samweli Laizer, amesema tangu Wizara ya Afya ilipotangaza uwepo wa Ebola katika nchi jirani za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mei 18, mwaka huu, mkoa umeimarisha ufuatiliaji katika maeneo ya mipaka, vituo vya afya, shule na sehemu nyingine zenye mikusanyiko ya watu.
Laizer amesema wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 700 wameendelea kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba, wakitoa elimu ya kujikinga dhidi ya Ebola na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo.
Amesema elimu hiyo pia inaendelea kutolewa katika shule, maeneo ya starehe, nyumba za ibada na mikusanyiko mingine ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha jamii inaendelea kuwa makini na kuchukua tahadhari zote muhimu dhidi ya ugonjwa huo.
Idara ya Afya mkoa wa Kagera imewahakikishia wananchi kuwa Mkoa wa huu unaendelea kuwa salama, huku ikisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi katika kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ni nguzo muhimu ya kuzuia kuingia na kusambaa kwa Ebola nchini.






Comments
Post a Comment