Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amefanya mazungumzo ya ngazi ya juu na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha elimu ya awali na msingi kwa mamilioni ya watoto duniani.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Seoul, Korea Kusini, ambapo Dkt. Kikwete yupo katika ziara ya kikazi kama Mwenyekiti wa Bodi ya Global Partnership for Education (GPE), taasisi ya kimataifa inayoratibu juhudi za kuongeza fursa za elimu katika zaidi ya nchi 90 duniani.
Katika mkutano huo, Dkt. Kikwete alimpongeza Ban Ki-moon kwa kuendelea kuwa kinara wa kuhamasisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora bila kujali mazingira anayokulia.
Aidha, alimshukuru kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya GPE na Serikali ya Korea Kusini, ambayo imeendelea kuwa miongoni mwa wadau muhimu wanaofadhili miradi ya elimu duniani.
Akizungumza katika mazungumzo hayo, Ban Ki-moon alisisitiza kuwa elimu ndiyo nyenzo yenye nguvu zaidi ya kuondoa umaskini, kukuza usawa na kujenga amani ya kudumu.
Amesimulia namna alivyonusurika katika athari za Vita ya Korea na jinsi msaada wa elimu na chakula kutoka Umoja wa Mataifa ulivyobadili maisha yake na kumwezesha kufikia nafasi ya juu ya uongozi duniani.
"Elimu ndiyo inayofungua milango ya matumaini na fursa kwa kila mtoto duniani," alisisitiza Ban Ki-moon.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kikwete pia alikutana na viongozi wa Serikali ya Korea Kusini pamoja na wabunge wanaoshughulikia elimu na ushirikiano wa maendeleo, ambao walieleza dhamira ya kuendelea kuunga mkono shughuli za GPE na kuongeza mchango wa kifedha katika Mkutano wa Ahadi wa GPE utakaofanyika Septemba mwaka huu mjini New York.
Kupitia kampeni ya GPE 2030, taasisi hiyo inalenga kukusanya dola za Marekani bilioni 15 kati ya mwaka 2026 na 2030 ili kuwezesha watoto takribani milioni 750 katika zaidi ya nchi 90 kupata elimu bora ya awali na msingi.
Tanzania inaendelea kunufaika na ushirikiano huo, ikiwa tayari imepokea zaidi ya dola za Marekani milioni 207.3 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu. Mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo yanatajwa kuiweka nchi katika nafasi nzuri ya kupata ufadhili zaidi katika miaka ijayo.
Mbali na mikutano ya viongozi, Dkt. Kikwete alitoa mhadhara wa wazi katika Chuo Kikuu cha Seoul National University, akisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo endelevu na njia bora ya kuandaa kizazi chenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.











Comments
Post a Comment