Na. Ssgt Mawazo Mtondo - DODOMA.
Kamishna wa Huduma za Urekebu Jeshi la Magereza, CP Amina Kavirondo, Julai 8, 2026, alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Jeshi la Magereza Jiji la Dodoma.
Katika ziara hiyo, CP Kavirondo alikagua eneo linalotarajiwa kujengwa Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza lililopo NCC Ntyuka lenye ukubwa wa hekari 7.3, eneo la ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza lililopo Itega lenye ukubwa wa hekari 4 na eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Makamishna lililopo Msalato.
Aidha, alikagua mradi wa ukarabati wa Gereza Maalum lililopo eneo la Isanga, mradi wa ujenzi wa Gereza Jipya linaloendelea kujengwa katika eneo la Msalato, ujenzi wa jukwaa la uwanja wa gwaride pamoja na jengo la kubadilishia nguo katika viwanja vya michezo vilivyopo eneo la Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato Jijini Dodoma.
Akiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa Gereza Jipya la Msalato, CP Kavirondo alisisitiza umuhimu wa kuchimbwa kisima kitakachosaidia upatikanaji wa maji kwa shughuli za ujenzi wa gereza hilo. Pamoja na hayo, aliwataka wataalamu wa ujenzi kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kubuni na kutekeleza miradi yenye ubora na ubunifu unaoweza kulitangaza Jeshi la Magereza ndani na nje ya nchi.
Katika ukaguzi wa viwanja vya michezo, CP Kavirondo aliwaelekeza wasimamizi wa mradi huo kufanya mawasiliano na wataalamu wa ujenzi wa viwanja vya michezo ili kuwasilisha mapendekezo ya kitaalamu yatakayowezesha ujenzi wa viwanja hivyo kuzingatia viwango vinavyokubalika na ubora unaohitajika.
Vilevile, CP Kavirondo alimuelekeza Mkuu wa Sehemu ya Ujenzi wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Kizito Jaka, kuendelea kutembelea miradi mbalimbali ya ujenzi iliyo jirani na Makao Makuu ya Jeshi la Magereza kwa lengo la kushauri mbinu bora za kitaalamu zitakazosaidia kuongeza ufanisi na ubora wa miradi inayotekelezwa na Jeshi hilo kupitia wataalamu wake wa ndani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sehemu ya Ujenzi Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Kizito Jaka, alimuhakikishia CP Amina Kavirondo kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yatatekelezwa kwa weledi na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.
Ziara hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Jeshi la Magereza, akiwemo Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, ACP George Wambura, wakuu wa gereza la Isanga na Msalato pamoja na wataalamu mbalimbali wa ndani ya Jeshi la Magereza.










Comments
Post a Comment