WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Mei 22, 2026, amesema mpango na bajeti ya wizara umeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa ikiwemo Dira ya Maendeleo 2050.
Amedema pia imezingatia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa (2026/2027–2030/2031), Ilani ya CCM ya mwaka 2025, sera na sheria mbalimbali, pamoja na maoni ya kamati za Bunge na maagizo ya viongozi wakuu wa serikali.
Aidha, Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, wizara itatekeleza vipaumbele vyake ambavyo ni kuendeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya viwanda, kuimarisha uzalishaji viwandani kupitia ujenzi wa kongani za viwanda (Industrial Clusters) na maeneo maalum ya viwanda (Industrial Estates) kwa viwanda vidogo na vya kati, pamoja na kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara kupitia ubunifu, teknolojia za kisasa na mafunzo ya ujuzi.
Amevitaja vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali, kuboresha mazingira ya biashara ili kukuza sekta binafsi, kuendeleza utafutaji wa masoko ya bidhaa na huduma za ndani, pamoja na kuanzisha Vituo vya Ubunifu na Ukuzaji wa Biashara kwa Vijana (Innovation and Business Hubs) vitakavyolenga kukuza ubunifu na ujasiriamali wa vijana.
Akifafanua zaidi, Mhe. Kapinga amesema vituo hivyo vitawawezesha vijana kupata nafasi ya kubuni na kukuza biashara zenye ushindani wa ndani na kimataifa, hususan katika kipindi hiki cha maendeleo ya kasi ya teknolojia na uchumi wa kidijitali, ambapo biashara za mtandaoni zinatarajiwa kukua kwa kasi zaidi na kuleta fursa kubwa kwa vijana nchini.

Comments
Post a Comment