SERIKALI kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imesema itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa kwa kuongeza uwekezaji katika zana za kisasa za kijeshi, teknolojia, mafunzo ya wanajeshi pamoja na upanuzi wa miundombinu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuwapa vijana wengi zaidi mafunzo ya kijeshi na stadi za kazi.
Kauli hiyo imetolewa na Dkt. Rhimo Nyansaho wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/27 leo Mei 19, 2026 Bungeni Jijini Dodoma.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, Wizara imepanga kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 (SDGs), pamoja na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika bajeti hiyo, Serikali inatarajia kutumia jumla ya Shilingi trilioni 4.28 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo, ambapo Shilingi trilioni 3.85 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida huku zaidi ya Shilingi bilioni 426 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Dkt. Nyansaho amesema sehemu kubwa ya fedha hizo itaelekezwa katika kuimarisha uwezo wa Jeshi kwa vifaa vya kisasa vya kijeshi, mifumo ya mawasiliano, mafunzo na rasilimali watu, sambamba na kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi ikiwemo huduma za afya, makazi, mazoezi na utunzaji wa vifaa vya kijeshi.
Aidha, Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha uwezo wa JKT kwa kuboresha miundombinu yake ili liweze kupokea na kutoa mafunzo kwa idadi kubwa zaidi ya vijana, huku Jeshi la Akiba nalo likiendelea kupewa nguvu kwa ajili ya kuongeza uwezo wa ulinzi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Serikali imeweka mkazo kwenye uanzishwaji wa viwanda vipya vya sekta ya ulinzi vitakavyozalisha bidhaa za matumizi ya kijeshi na kiraia, pamoja na kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi katika uwekezaji wa viwanda hivyo.
Pia, Wizara imeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya ulinzi kupitia Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki, sambamba na kuendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura mbalimbali nchini.









Comments
Post a Comment