Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewasilisha bungeni jijini Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi trilioni 2.564 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Akiwasilisha bajeti hiyo leo Mei 20, 2026, Ulega amesema fedha hizo zitalenga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, jumla ya shilingi bilioni 97.1 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida ya Wizara na taasisi zake, ambapo shilingi bilioni 92.2 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi huku shilingi bilioni 4.8 zikielekezwa kwenye matumizi mengine ya uendeshaji.
Aidha, shilingi trilioni 2.467 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo kati ya fedha hizo shilingi trilioni 1.544 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 922.4 ni fedha za nje.
Serikali imeeleza kuwa fedha hizo zitatumika katika ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya barabara nchini kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri, kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kufungua fursa zaidi za maendeleo kwa wananchi.


Comments
Post a Comment