WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amefanya mazungumzo na Wakuu wa Mikoa sita ya mipakani nchini katika kikao kilichofanyika tarehe 20 Mei 2026, Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo – Dodoma, kikilenga kuimarisha mikakati ya pamoja ya ulinzi na usalama wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa mikoa ya kimkakati inayopakana na mataifa jirani, ambapo walijadili kwa kina masuala ya usalama wa mipaka, udhibiti wa changamoto za kiusalama, pamoja na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za ulinzi na uongozi wa mikoa katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu.
Wakuu wa Mikoa waliohudhuria ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makalla; Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Burian; Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Mtambi; Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabir Makame; Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Kanali Yahya Kido; pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Donald Msengi.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Dkt. Nyansaho amesisitiza kuwa usalama wa mipaka ni msingi muhimu wa ustawi wa taifa, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha uratibu wa karibu kati ya Wizara ya Ulinzi, Jeshi la Kujenga Taifa na viongozi wa mikoa ya mipakani ili kuongeza ufanisi katika ulinzi wa nchi.
Aidha, viongozi hao wa mikoa walipata fursa ya kutembelea Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa na kujionea kwa karibu mifumo ya uratibu na utekelezaji wa shughuli za ulinzi wa taifa, hatua iliyowasaidia kupata uelewa wa kina kuhusu namna taasisi hiyo inavyofanya kazi.









Comments
Post a Comment