Skip to main content

Wanawake wamiliki asilimia 54 ya biashara ndogo nchini

šŸ“TRA yawawekea mkakati rafiki wa Kodi 

Na MASHAKA MHANDO, Tanga

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga, imebainisha kuwa wanawake nchini wanamiliki asilimia 54 ya biashara ndogo, za kati na ndogo (MSMEs), hali inayolazimu kuwepo kwa mifumo rafiki ya kodi itakayochochea ukuaji wa sekta hiyo bila hofu ya vikwazo.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 14, 2026, na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, John Castro wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi lililofanyika katika ukumbi wa Regal Naivera Hotel jijini hapa.



John alisema takwimu za hivi karibuni zinaonyesha mchango mkubwa wa wanawake katika uchumi, ambapo ushiriki wao katika nguvu kazi unakadiriwa kufikia takribani asilimia 80 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jambo linalowafanya kuwa mhimili mkuu wa mapato ya ndani.


Jukwaa la Wanawake na Kodi

Meneja huyo alifafanua kuwa kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni hatua ya kihistoria yenye lengo la kuwapa wanawake elimu sahihi, kusikiliza changamoto zao, na kujenga uaminifu utakaohamasisha ulipaji kodi kwa hiari badala ya kutumia nguvu.

"Tunatambua kuwa mwanamke akisimama kiuchumi, familia inaimarika na Taifa linapiga hatua. TRA imejikita kuboresha huduma kwa weledi na uwazi ili mwanamke ajisikie salama na anaheshimiwa anaposhiriki katika mfumo wa kodi," alisema John.


Kodi na Miradi ya Kimkakati

John alisisitiza kuwa kodi ndiyo injini inayogharamia miradi ya kimkakati nchini ikiwemo afya, elimu, barabara na maji, hivyo mwanamke anayelipa kodi anakuwa mshirika wa moja kwa moja wa Serikali katika ujenzi wa Taifa.

Aidha, aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Tanga chini ya Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian na wadau wa maendeleo kama GIZ, kwa kuweka mazingira yanayowawezesha   kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kupata elimu ya kodi.


Wito kwa Wadau na Taasisi za Fedha

Katika kongamano hilo, TRA imetoa wito kwa taasisi za kifedha kushirikiana na Mamlaka hiyo wakati wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wanawake, ili waweze kupewa elimu ya kodi sambamba na mitaji, jambo litakalosaidia biashara zao kuimarika na kuwa endelevu.

Pia, aliwataka wanawake wote mkoani Tanga kujisajili katika mfumo wa kodi na kutumia madawati ya uwezeshaji biashara yaliyopo katika kila ofisi ya TRA ili kupata ushauri wa kitalamu wa kibiashara.

Mmoja ya washiriki wa kongamano Hilo, kutoka kampuni ya Maluu Smart Production, Hadija Mohamed, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga kwa kuanzisha jukwaa hilo, akisema limekuwa mkombozi katika kufungua macho ya wanawake wajasiriamali kuhusu mnyororo wa kodi na fursa za kibiashara. Hadija amebainisha kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuendesha biashara zao kwa weledi na kuondoa hofu ya awali waliyokuwa nayo dhidi ya kodi, jambo litakalopelekea uzalishaji wenye tija na kufuata sheria za nchi kitalamu.

Aidha, Hadija amesisitiza kuwa kupitia mafunzo hayo, Maluu Smart Production imejipanga kuwa balozi wa utii wa kodi kwa hiari, huku akiiomba TRA kuendelea kutoa huduma za ushauri wa karibu kwa viwanda vidogo ili viweze kukua na kufikia soko la kimataifa. Amesema kuwa kutambuliwa kwa mchango wa mwanamke katika uchumi kupitia kongamano hilo ni ishara tosha ya ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza mapato ya ndani na maendeleo ya kijamii. 

Comments

George marato tv

RAIS RUTTO AAMBATANA NA ODINGA NCHINI CHINA

Rais wa Jamhuri ya Kenya Mh William Rutto na mke wake wamewasili nchini China kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Katika ziara hiyo ameambatana na waziri mkuu mstaafu wa nchi hiyo Raila Odinga ambaye pia anapigiwa kampeni ili aweze kushinda nafasi ya Uenyekiti wa AU.

WIZARA YA MALI ASILI YASISITIZA MATUMIZI YA SHERIA NA KANUNI KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UHIFADHI

Na.Joyce Ndunguru, Morogoro. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba asisitiza matumizi ya sheria na kanuni katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uhifadhi. Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo leo Septemba 1, 2024 wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kuongea na watumishi ili kuimarisha utendaji kazi pamoja na kukagua maeneo ya kazi. "Kama wahifadhi tunapaswa kufahamu sheria zote zinazosimamia masuala ya uhifadhi zilizopo katika Taasisi zetu pamoja na za Taasisi zingine za uhifadhi zilizopo ndani ya Wizara ya Maliasili na utalii" amesema Kamishna Wakulyamba. "Pamoja na kufahamu sheria na kanuni zilizopo ndani ya Wizara yetu, ni vyema kufahamu na kuzingatia sheria nyingine za Nchi ambazo zinatuzunguka ili ziweze kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu mfano sheria inayohusiana na ukusanyaji wa vielelezo kuanzia kw...

Rais Dkt. Samia Awasili China Kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano Kati ya China na Africa FOCAC

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Beijing Capital nchini China kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) tarehe 03 Septemba, 2024.