Wananchi wa Kijiji Cha Burunga Wampongeza Rais Samia Kwa Mradi Wa Kiwanja Cha Ndege Cha Kimataifa Serengeti
WANANCHI wa kijiji cha Burunga wilayani Serengeti Mkoani Mara wamepongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wa kuidhinisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti, wakisema mradi huo utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uchumi, biashara na ajira katika eneo hilo.
Pongezi hizo zimekuja baada ya Serikali kupitia Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kueleza hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati unaotarajiwa kuongeza ukuaji wa sekta ya utalii nchini huku ukilinda mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Baadhi ya wakazi wa Burunga akiwemo Mzee Joseph Charles,Mboyi Mremi Mancha pamoja na Benjamini Jumanne Kairo, wamesema ujenzi wa kiwanja hicho ni neema kubwa kwa wananchi wa Serengeti kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa watalii na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Wamesema kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa nyingi za biashara kwa wananchi ikiwemo huduma za malazi, usafiri, biashara ndogo ndogo pamoja na ajira kwa vijana, jambo litakalosaidia kuongeza kipato cha familia nyingi.
“Watalii wengi watakuwa wanashuka moja kwa moja hapa Serengeti, hivyo biashara zitapanuka na wananchi watanufaika kiuchumi,” walisema wakazi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa hatua yake ya kihistoria ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti, akisema mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Amesema uamuzi huo ni matokeo ya maono ya muda mrefu ya wadau wa utalii, viongozi wa serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mara waliokuwa wakisisitiza umuhimu wa kuboreshwa kwa miundombinu ya usafiri katika eneo la Serengeti.
Aidha,Amefafanua kuwa kwa sasa uwanja mdogo uliopo Serengeti ni miongoni mwa viwanja vinavyotumika kwa wingi zaidi nchini, ambapo kwa baadhi ya siku hupokea takribani ndege mia moja mchana pekee, hali inayoonesha wazi uhitaji mkubwa wa uwanja wa kisasa wa kimataifa utakaoendana na hadhi ya eneo hilo.
“Serengeti ni hazina ya kipekee duniani, ni Urithi wa Dunia uliosajiliwa na UNESCO, na ni miongoni mwa maeneo yanayovutia watalii kutoka kila pembe ya dunia kutokana na maajabu ya uhamaji wa wanyama pori na mandhari yake ya kipekee,” amesema Mtambi.
Katika maelezo yake bungeni wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara ya Uchukuzi, waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mabara alisema Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa anga, kukuza utalii na kupunguza changamoto ya uwepo wa viwanja vingi ndani ya hifadhi.
Serikali imebainisha kuwa hadi kufikia Machi 2026 hatua ya awali ya uchambuzi wa sifa za wakandarasi wa kimataifa (Pre-qualification) imekamilika na kwa sasa taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi pamoja na mhandisi mshauri zinaendelea.









Comments
Post a Comment