Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tanzania inatarajiwa kupokea ujumbe mkubwa wa viongozi wa elimu ya juu kutoka Malaysia, wakiwemo viongozi kutoka Wizara ya Elimu ya Malaysia, Education Malaysia Global Services (EMGS), pamoja na wawakilishi wa vyuo vikuu tisa vitakavyoshiriki Maonesho ya Elimu ya Malaysia yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 1 hadi 3, 2026 katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.
Ujumbe huo wa watu 19 kutoka Malaysia unatarajiwa kuwasili nchini tarehe ikiwa ni maandalizi ya kushiriki maonesho hayo pamoja na kufanya vikao vya kimkakati na wadau mbalimbali wa elimu nchini, ikiwemo Wizara ya Elimu, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), vyuo vikuu vya Tanzania, shule, wazazi, walezi na wanafunzi.
Maonesho hayo, yanayoratibiwa kwa ushirikiano wa Global Education Link (GEL) na wadau wa elimu kutoka Malaysia, yanalenga kufungua fursa za udahili, ufadhili wa masomo, ushirikiano wa kitaaluma, pamoja na kuimarisha mahusiano ya elimu ya juu kati ya Tanzania na Malaysia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdumalik Mollel, alisema ujio huo ni wa kimkakati kwa Tanzania kwa kuwa unahusisha mamlaka muhimu za elimu ya juu kutoka Malaysia, vyuo vikuu, pamoja na taasisi zinazoratibu masuala ya wanafunzi wa kimataifa, ikiwemo taratibu za udahili na visa.
Bwana Mollel alisema ujumbe huo utajumuisha viongozi kutoka Wizara ya Elimu ya Malaysia, viongozi wa EMGS na wawakilishi wa vyuo vikuu tisa ambavyo vitatoa taarifa za moja kwa moja kuhusu programu za masomo, gharama, mazingira ya kujifunzia, taratibu za udahili na nafasi za scholarship kwa wanafunzi wa Tanzania.
“Hii siyo exhibition ya kawaida ya udahili pekee. Ni fursa ya kitaifa ya kuunganisha Tanzania na Malaysia katika elimu ya juu, scholarship, programu za pamoja, tafiti, ubunifu na makubaliano ya ushirikiano kati ya vyuo vya pande zote mbili,” alisema Bwana Mollel.
Alisema miongoni mwa taasisi zinazotarajiwa kushiriki ni Asia Pacific University of Technology and Innovation (APU), University of Malaya, University Putra Malaysia (UPM), University Kebangsaan Malaysia (UKM), UCSI University, University Kuala Lumpur, University Selangor (UNISEL) na Putra Business School, huku taasisi nyingine zikitarajiwa kuthibitishwa kupitia mwongozo rasmi wa maonesho.
Kwa mujibu wa Bwana Mollel, ujio wa vyuo hivyo ni fursa kubwa kwa wanafunzi wa Tanzania wanaotafuta elimu ya kimataifa katika maeneo ya sayansi, teknolojia, biashara, afya, uhandisi, TEHAMA, ubunifu, ujasiriamali na taaluma nyingine zenye mahitaji makubwa katika soko la ajira la sasa na la baadaye.
Alisema tofauti na maonesho mengine ya elimu, ujumbe huu umebeba agenda pana inayohusisha ushirikiano wa kitaasisi kati ya vyuo vya Malaysia na vyuo vya Tanzania. Alibainisha kuwa vyuo vya Malaysia vimeonyesha utayari wa kusaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano, yaani MoU, na vyuo vya Tanzania vitakavyokuwa tayari kushirikiana katika maeneo ya tafiti, ubadilishanaji wa wanafunzi na wahadhiri, programu za pamoja, mafunzo ya muda mfupi, teknolojia na ubunifu.
“Vyuo vya Malaysia vipo tayari kukutana na vyuo vya Tanzania. Vipo tayari kusikiliza mahitaji ya vyuo vyetu na kuona namna ya kujenga ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili. Hii ni nafasi nzuri kwa vyuo vyetu kujiunganisha na mfumo wa elimu wa kimataifa,” alisema Bwana Mollel.
Aliongeza kuwa ujumbe huo pia upo tayari kufanya kikao cha pamoja na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania, ambapo vyuo vya Malaysia vitapata nafasi ya kufanya mawasilisho mafupi kuhusu programu zao, malengo yao nchini Tanzania na maeneo wanayotaka kushirikiana na Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania, baadhi ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zitapata nafasi ya kueleza maeneo yao ya kipaumbele katika ushirikiano, ikiwemo programu za “2+2”, tafiti za pamoja, mafunzo ya kitaaluma, ubunifu, ujasiriamali na kuimarisha mahusiano ya kitaaluma kati ya Tanzania na Malaysia.
Mollel alisema maonesho hayo yana umuhimu mkubwa pia kwa Wizara ya Elimu nchini Tanzania, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Kamati ya Samia Suluhu Hassan Scholarship Scheme, shule, wazazi, walezi na vijana kwa ujumla, kwa kuwa yatafungua majadiliano ya moja kwa moja kuhusu nafasi za ufadhili wa masomo na ushirikiano wa elimu ya juu.
Alisema kwa Wizara ya Elimu, ujio huo ni fursa ya kujenga daraja la mahusiano ya kitaaluma kati ya Tanzania na Malaysia, hasa katika eneo la elimu ya juu, ubora wa programu, utaratibu wa wanafunzi wa kimataifa na mifumo ya kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.
Kwa TCU, Bwana Mollel alisema maonesho hayo yanaweza kufungua nafasi ya kubadilishana uzoefu na mamlaka za elimu ya juu kutoka Malaysia kuhusu usimamizi wa ubora, ithibati, uendelezaji wa programu za pamoja na uratibu wa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi.
Aidha, alisema Kamati ya Samia Suluhu Hassan Scholarship Scheme nayo inaweza kutumia ujio huo kujadiliana na vyuo vya Malaysia kuhusu uwezekano wa kuongeza nafasi za scholarship kwa Watanzania, hususan katika taaluma zenye umuhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Tunataka Study in Malaysia Exhibition iwe mwanzo wa safari mpya ya ushirikiano wa elimu kati ya Tanzania na Malaysia. Hii ni fursa ya udahili, lakini pia ni fursa ya diplomasia ya elimu, maendeleo ya vijana na ujenzi wa rasilimali watu kwa taifa,” alisema Bwana Mollel.





Comments
Post a Comment