Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya barabara na flyovers katika majiji na miji mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha usafiri mijini na kupunguza msongamano wa magari.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi bungeni jijini Dodoma leo Mei 20, 2026, Ulega amesema miradi hiyo pia inalenga kuongeza tija ya kiuchumi, kurahisisha shughuli za usafirishaji na kuinua ubora wa maisha ya wananchi.
Amesema miradi hiyo itatekelezwa katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma pamoja na miji ya Pwani Region, Iringa na Singida.
Kwa upande wa Dar es Salaam, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara pamoja na flyovers katika maeneo mbalimbali ili kupunguza adha ya foleni ambayo imekuwa ikichangia upotevu wa muda na kuchelewesha shughuli za kiuchumi.
Katika Jiji la Dodoma, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje yenye urefu wa kilometa 112.3 ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, huku ikitarajiwa kusaidia kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji hilo la makao makuu ya nchi.
Aidha, Serikali imeendelea na upanuzi wa barabara ya Arusha–Kisongo katika Jiji la Arusha kutoka njia mbili hadi nne, wakati Mwanza ikitarajia kuanza upanuzi wa barabara ya Mwanza–Usagara pamoja na maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Mwanza Airport–Kayenze.
Kwa upande wa Mbeya, Serikali inaendelea na upanuzi wa barabara ya Nsalaga–Uyole–Ifisi pamoja na maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Uyole–Songwe, huku miradi mingine ya miundombinu ikiendelea katika miji ya Iringa na Singida.


Comments
Post a Comment