Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali inafikiria kuzifanya Mbio za Siku ya Afrika kuwa za kimataifa ili kufanikisha lengo la kuleta maendeleo ya pamoja kwa bara la Afrika.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mbio hizo jijini Dar es Salaam Mei 23, 2026, Mhe. Makonda alisema mbio hizo zimeendelea kuwa alama ya umoja, mshikamano na maendeleo ya Waafrika.
Alisema Serikali inalenga kukuza mbio za Siku ya Afrika ili ziwe jukwaa la kimataifa litakalokutanisha Waafrika kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano na diplomasia kupitia michezo.
Akizungumzia mshikamano na uwajibikaji wa Waafrika, Waziri Makonda alisema hakuna Mtu atakayekuja kutupa hela ili kuijenga au kuilinda Tanzania na Afrika isipokuwa Waafrika wenyewe na kusisitiza kuwa ni wajibu wa Watanzania na Waafrika kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha wanailinda na kuiendeleza Afrika kwa kutumia nguvu, umoja na rasilimali walizonazo.
“Sisi ni Waafrika, tunapaswa kujivunia bara letu na kufanya kazi kwa pamoja kwa sababu hakuna mtu atakayekuja kutupa fedha, wala hakuna atakayekuja kulinda bara letu. Hakuna atakayekuja kutulindia nchi yetu wala kuilinda Afrika isipokuwa sisi wenyewe. Afrika kwa sasa inapiga hatua kubwa na ina uwezo mkubwa wa kufanikiwa kutokana na rasilimali, nguvu kazi na umoja wa watu wake.”
Aliwaasa Watanzania na Waafrika kutumia kipindi hiki kama fursa ya kuimarisha mshikamano kwa ajili ya kulinda mustakabali wa bara la Afrika kuhakikisha jamii zinakuwa salama na zenye maendeleo endelevu.


















Comments
Post a Comment