WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ameliambia Bunge jijini Dodoma Mei 15, 2026 kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kutumia fursa ya Shindano la 74 la Ulimbwende wa Dunia (Miss World 2027) katika kuimarisha na kutangaza sekta ya utalii kimataifa.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Kijaji amesema mashindano hayo makubwa duniani, yatakayofanyika Mei 2027 nchini Tanzania, yanatarajiwa kuvutia washiriki 120 kutoka mataifa mbalimbali pamoja na wageni takriban 20,000, hatua itakayolifanya taifa kuwa kitovu cha macho ya dunia.
Ameeleza kuwa tukio hilo ni fursa muhimu ya kipekee kwa Tanzania kujitangaza kimataifa kupitia vivutio vyake vya utalii, utamaduni na urithi wa asili, hivyo kuongeza mapato na idadi ya watalii wanaotembelea nchi.
Katika maandalizi hayo, Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) itawahamasisha wadau wa sekta ya utalii kuandaa na kuuza vifurushi vya safari kupitia majukwaa ya kidijitali ya TTB (booking platforms). Sambamba na hilo, mashindano yatatangazwa kupitia tovuti rasmi, mitandao ya kijamii, televisheni, redio na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Aidha, Wizara itaratibu ziara za mafunzo (FAM Trips) kwa walimbwende na waandishi wa habari kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kabla ya mashindano, ili kuongeza uelewa na kueneza taswira chanya ya Tanzania kimataifa kupitia maudhui yatakayozalishwa na kusambazwa duniani.
Vilevile, mabanda ya utalii yatawekwa katika maeneo yatakapofanyika mashindano ili kutoa taarifa na elimu kwa wageni, huku maudhui yatakayozalishwa wakati wa tukio hilo yakitumika kuimarisha zaidi utambulisho wa Tanzania kimataifa.
Baada ya mashindano, Wizara kwa kushirikiana na wadau itaratibu ziara za utalii kwa wageni kupitia mfumo wa TTB, sambamba na kuwateua washindi watano wa juu wa Miss World 2027 kuwa mabalozi wa hiari wa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania duniani.










Comments
Post a Comment