TANZANIA inatarajiwa kunufaika kiuchumi na kijamii kupitia uenyeji wa Miss World 2027, tukio kubwa la kimataifa linalotarajiwa kuvutia maelfu ya wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Mashindano hayo yanatajwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta za utalii, biashara, ubunifu na ajira, huku pia yakiitangaza nchi kimataifa kama kitovu cha utamaduni na vivutio vya asili.
Mafanikio hayo yamebainishwa Bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake uliowezesha Tanzania kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
“Mheshimiwa Spika, natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake madhubuti ulioiwezesha Tanzania kupata heshima hii kubwa ya kimataifa,” alisema Waziri Makonda.
Ameongeza kuwa:“Mashindano haya yataleta mapato kupitia utalii, udhamini na biashara za wageni, huku yakitoa fursa kwa wabunifu wa ndani kujifunza na kujitangaza kimataifa.”
Aidha, Mhe Makonda ameeleza kuwa maandalizi ya uenyeji huo yanaendelea kupitia mashindano ya Miss World Tanzania 2026, ambapo mlimbwende Latricia Ian Sawe aliibuka mshindi na anatarajiwa kuiwakilisha Tanzania nchini Vietnam.
“Huu ni mwanzo wa safari ya kuelekea kupokea rasmi bendera ya uenyeji wa Miss World 2027,” amesisitiza.
Pia amebainisha kuwa tukio hilo litaongeza hamasa ya kitaifa kuelekea maandalizi ya AFCON 2027, “Miss World 2027 itakuwa kichocheo muhimu cha mshikamano wa kitaifa na ushiriki wa wananchi katika matukio makubwa ya kimataifa.”



Comments
Post a Comment