Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo ametoa tracksuit 25 za mazoezi kwa wanafunzi mbalimbali wa shule za msingi waliopo kwenye kambi ya maandalizi ya mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya mkoa na baadaye taifa.
Kambi hiyo ya maandalizi imewekwa katika Shule ya Msingi Dareda kati wilayani Babati, ambapo wanafunzi hao wanaendelea kujifua kwa ajili ya kuiwakilisha Halmashauri ya Wilaya ya Babati katika mashindano hayo muhimu ya michezo na sanaa.
Tracksuit hizo zimekabidhiwa kwa niaba ya mbunge huyo na Katibu wa Mbunge, Waziri Juma, ambaye amewatakia kila la heri wanafunzi hao wanapojiandaa kwenda kushindana na wenzao kutoka halmashauri mbalimbali za mkoa na taifa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Waziri Juma amesema Mheshimiwa Sillo anaendelea kuthamini michezo kama sehemu muhimu ya kukuza vipaji vya watoto, kuimarisha afya pamoja na kujenga nidhamu kwa wanafunzi.
“Mheshimiwa Daniel Sillo anaamini michezo ni njia muhimu ya kukuza vipaji na kuwajenga watoto kuwa na nidhamu, kujiamini na kutimiza ndoto zao,” amesema Waziri Juma.
Kwa upande wao, wanafunzi pamoja na walimu waliopo kambini wamemshukuru Mbunge Daniel Sillo kwa kuendelea kuunga mkono michezo na kuwapatia mahitaji muhimu yatakayowasaidia kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.
Michezo inayoshindaniwa katika UMITASHUMTA mwaka huu ni pamoja na mpira wa miguu, netiboli, volleyball, riadha, mpira wa goli kwa wenye uoni hafifu pamoja na sanaa za jukwaani.
Afisa Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Ramadhan Mnyoti amesema halmashauri hiyo imeendelea kufanya vizuri kimichezo ambapo kwa miaka minne mfululizo imekuwa bingwa wa mkoa.
Amesema jumla ya wanafunzi 120 kutoka shule zote za msingi 165 za Halmashauri ya Wilaya ya Babati zinashiriki katika maandalizi hayo kwa ajili ya kuipeperusha vyema bendera ya wilaya hiyo kwenye mashindano ya UMITASHUMTA.






Comments
Post a Comment