Mageuzi ya elimu nchini yanahitaji mfumo imara wa kisheria utakaowezesha utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023 na mitaala iliyoboreshwa.
Hayo yameelezwa Mei 21, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika Kikao cha kujadili taarifa ya awali ya mapitio ya Sheria ya Elimu Sura 353 ambapo amesema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mageuzi ya elimu yameweka msingi wa maboresho ya sera, mitaala na sheria.
Amebainisha kuwa tayari timu ya wataalamu imekamilisha kazi ya awali ya mapitio, na sasa Wizara inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau ili kukamilisha mchakato huo na kuwezesha kuwasilisha mapendekezo katika ngazi mbalimbali ngazi za maamuzi.
Aidha, amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wadau wote wa elimu ikiwemo hivyo amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji mpana katika kutoa maoni kwa ajili ya mapitio ya Sheria.
"Mhe. Rais alielekeza mageuzi yote yanayofanyika katika sekta ya elimu yashirikishe wadau" Amesema Prof. Mkenda.
Amewahakikishia wadau kuwa milango ya Wizara ipo wazi kupokea maoni na kuwataka viongozi wote wa Wizara kuhakikisha maoni wanayopokea kuwasilisha kwa kamati husika.
Waziri Mkenda amesema kuwa zoezi la mapitio limechukua muda mrefu ili kutoa fursa Kwa Kila mdau kushiriki kutoa maoni. Ameshukuru na kuwapongeza wadau wote walioshiriki kuwezesha zoezi hili kutoka sekta za umma, wadau wa maendeleo na sekta binafsi.




Comments
Post a Comment