Abiria na wadau wa usafiri wa reli nchini wameeleza namna huduma ya reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) ilivyokuwa chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, biashara, usafirishaji wa mizigo, utunzaji wa mazingira pamoja na kuokoa muda kwa wananchi.
Maoni hayo yametolewa wakati wa kampeni ya #NusuMudaKoteKote iliyoandaliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa lengo la kuadhimisha miaka miwili tangu kuanza kwa huduma ya SGR nchini.
Wadau hao wamesema ujio wa reli hiyo umeleta mageuzi makubwa katika mfumo wa usafiri wa Tanzania kwa kutoa huduma ya kisasa yenye kasi, usalama na ufanisi mkubwa ukilinganisha na mifumo mingine ya usafiri.
Katika kampeni hiyo, TRC imeeleza kuwa #NusuMudaKoteKote inalenga kuhamasisha matumizi ya reli ya kisasa ya SGR pamoja na kuonyesha mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa huduma hiyo miaka miwili iliyopita pamoja na kuonesha namna SGR ilivyopunguza muda wa safari, kuongeza ufanisi wa shughuli za wananchi na kuboresha huduma za usafiri nchini kupitia kaulimbiu ya “Safiri, Fanya Kazi, Fika Haraka.”
Aidha, wananchi na wadau mbalimbali wamepongeza mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia na kuendeleza mradi wa reli ya kisasa nchini.
Wamesema uwekezaji unaoendelea kufanywa katika SGR umeongeza matumaini ya wananchi juu ya maendeleo ya sekta ya usafiri na uchumi kwa ujumla.
“Leo Tanzania tunajivunia kuwa na reli ya kisasa inayokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia duniani. Haya ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali,” alisema mmoja wa wadau waliohudhuria uzinduzi huo.
Kwa upande wa utalii, wadau wameeleza kuwa SGR imeongeza urahisi wa kusafiri kati ya mikoa mbalimbali na hivyo kufungua fursa zaidi kwa watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo tofauti kwa muda mfupi na gharama nafuu.
Wameeleza kuwa reli hiyo imekuwa kivutio pia kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaotamani kupata uzoefu wa usafiri wa kisasa unaofanana na ule wa nchi zilizoendelea.
Katika sekta ya biashara, wadau wamebainisha kuwa SGR imeongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi kwa kurahisisha usafiri wa wafanyabiashara pamoja na usafirishaji wa bidhaa na mizigo kutoka eneo moja kwenda jingine kwa haraka zaidi.
“Leo mfanyabiashara anaweza kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa shughuli zake na kurejea siku hiyo hiyo. Hii inaongeza tija na kuokoa gharama,” alisema mmoja wa wadau hao.
Aidha, wadau hao wameeleza kuwa matumizi ya reli ya umeme yana mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira kutokana na kupunguza matumizi ya mafuta pamoja na msongamano wa magari barabarani.
Wamebainisha kuwa kuongezeka kwa matumizi ya SGR kutasaidia kupunguza hewa chafuzi zinazotokana na usafiri wa magari mengi ya barabarani, hatua ambayo ni muhimu katika kulinda mazingira na afya za wananchi.
Kwa upande wa muda, abiria mbalimbali wameeleza kuwa reli hiyo imekuwa suluhisho kwa changamoto za ucheleweshaji wa safari zilizokuwa zikisababishwa na foleni pamoja na uchovu wa safari za barabarani.
“SGR imefanya safari kuwa rahisi, salama na ya haraka. Unaweza kusafiri na kufika mapema bila kuchoka,” alisema mmoja wa abiria.
Wadau hao pia wameeleza kuwa huduma ya SGR imeendelea kusaidia usafirishaji wa mizigo kwa ufanisi mkubwa, jambo linalorahisisha shughuli za biashara na kuongeza ushindani wa kiuchumi ndani na nje ya nchi.
Kupitia kampeni hiyo, TRC imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kutumia usafiri wa reli ya kisasa kutokana na kasi yake, usalama, mchango wake katika maendeleo ya uchumi pamoja na uwezo wake wa kuokoa muda kwa wasafiri na wafanyabiashara.








