NAIBU Waziri Ofisi ya waziri Mkuu tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) Festo Dugange ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kasi katika kuboresha miundombinu ya barabara katika Jimbo la Butiama, ambapo jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 5.33 zimetengwa katika miaka miwili ya fedha kwa ajili ya matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara, madaraja na makalvati.
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Butiama Mheshimiwa Dkt. Wilson Charles Mahera, leo Mei 12,2026 Bungeni Jijini Dodoma, aliyetaka kujua Je, ni lini Serikali itaanza na kukamilisha utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa Barabara katika Jimbo la Butiama.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Mhe. Festo Dugange amesema Serikali imejipanga kuhakikisha mtandao wa barabara wa wilaya ya Butiama wenye urefu wa kilomita 596.62 unaboreshwa ili kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Wilaya ya Butiama ina mtandao wa barabara wa kilomita 596.62 unaohudumiwa na TARURA. Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara mbalimbali ambapo kila mwaka bajeti imeendelea kuongezeka,” ameeleza
Amesema Serikali, katika mwaka wa fedha 2025/2026, Butiama ilitengewa shilingi bilioni 2.59 kwa ajili ya matengenezo ya barabara maeneo korofi, pamoja na ujenzi wa madaraja 14 na makalvati 26, ambapo zaidi ya shilingi milioni 722.6 tayari zimepelekwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga shilingi bilioni 2.74 kwa ajili ya kuendeleza matengenezo na ukarabati wa barabara, pamoja na ujenzi wa madaraja 17 na makalvati 29.
“Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa barabara za Wilaya ya Butiama ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi,” amesisitiza.
Akiuliza swali la Nyongeza Mbunge wa Butiama Mhe. Dkt. Wilson Charles Mahera, ameeleza changamoto za miunganisho ya barabara katika kata za Kianyari, Masaba, Sirori Simba na Buswahili, akibainisha kuwa baadhi ya maeneo bado hayana mtandao imara wa barabara licha ya mahitaji makubwa ya kijamii na kiuchumi.
Akijibu swali hilo la Nyongeza Naibu waziri TAMISEMI Mhe. Festo Dugange amesema Serikali imekiri kuwepo kwa maeneo ambayo bado hayajaunganishwa kikamilifu, na kueleza kuwa TARURA inaendelea kupanga vipaumbele vya kufungua na kuboresha barabara hizo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Aidha, Amesema Serikali imethibitisha kupokea maombi ya takribani shilingi bilioni 1.382 kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizoathiriwa na mvua katika maeneo mbalimbali ya Butiama, ikiwemo barabara za Butiama,Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kyabakari, Kamugegi, Sirori Simba na maeneo mengine.
“Maeneo yote yaliyoainishwa yatazingatiwa katika mipango ya bajeti ya awamu zijazo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri na usafirishaji,”. Ameeleza
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha mtandao wa barabara nchini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika maeneo ya vijijini kama Butiama.

