Serikali Yasifiwa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti, Wasema ni Mageuzi Makubwa ya Utalii na Uchumi
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa hatua ya kihistoria ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti, akisema mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Amesema uamuzi huo ni matokeo ya maono ya muda mrefu ya wadau wa utalii, viongozi wa serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mara waliokuwa wakisisitiza umuhimu wa kuboreshwa kwa miundombinu ya usafiri katika eneo la Serengeti.
Aidha, amesema uwanja mdogo uliopo Serengeti kwa sasa ni miongoni mwa viwanja vinavyotumika kwa wingi nchini, ambapo kwa baadhi ya siku hupokea takribani ndege mia moja mchana pekee, hali inayoonesha wazi uhitaji mkubwa wa uwanja wa kisasa wa kimataifa utakaoendana na hadhi ya eneo hilo.
Mtambi ameongeza kuwa Serengeti ni hazina ya kipekee duniani, Urithi wa Dunia uliosajiliwa na UNESCO, na moja ya maeneo yanayovutia watalii kutoka kila pembe ya dunia kutokana na uhamaji wa wanyama pori na mandhari yake ya kipekee.
Nao baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Burunga wilayani Serengeti mkoani Mara wameipongeza Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa uamuzi wa Serikali wa kuendelea na mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti, wakisema mradi huo ni chachu ya maendeleo na fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
Miongoni mwa wananchi hao ni Steven Benjamin pamoja na mzee philipo manyanya ambapo wamesema wanayomfuraja kubwa sana kuona maandalizi ya ujenzi wa kiwanja hicho yanaendelea chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Sisi tuna furaha sana kuona uwanja wa ndege unaanza kujengwa hapa. Hii ni fursa kubwa kwa wananchi wa Serengeti na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya uamuzi huu mkubwa wa maendeleo,” amesema Benjamin
Wamesema eneo la Serengeti ni kitovu cha utalii hivyo uamuzi wa kujenga kiwanja hicho katika eneo hilo ni sahihi na utasaidia wananchi kunufaika moja kwa moja na rasilimali ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Hapa ndiyo kitovu cha utalii, kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kujenga uwanja huu. Utasaidia wananchi wa Serengeti kuona faida ya uwepo wa hifadhi yetu,” wamesema.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza ukuaji wa sekta ya utalii nchini sambamba na kulinda mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia mfumo wa “Green Airport” unaozingatia utunzaji wa mazingira.







Comments
Post a Comment