WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika utekelezaji wa miradi ya barabara nchini, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wanawake wanapata nafasi zaidi katika sekta ya ujenzi na miundombinu.
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Mei 20, 2026, Ulega amesema kupitia Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake, Wizara imeendelea kufanya maboresho ya kanzidata maalum inayohifadhi na kufuatilia taarifa za ushiriki wa wanawake katika miradi ya barabara ili kuongeza ufanisi wa usimamizi na ufuatiliaji.
Amesema sambamba na hatua hiyo, Serikali imeendelea kuboresha mwongozo wa ushirikishwaji wa wanawake katika sekta ya ujenzi kwa lengo la kutoa mwelekeo sahihi kwa wadau wote kuhusu namna bora ya kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo.
“Kitengo pia kimeendelea kufanya ukaguzi wa kazi zinazotekelezwa na wakandarasi wanawake katika mikoa mbalimbali ili kuhakikisha ubora wa kazi pamoja na kuimarisha usawa wa fursa katika utekelezaji wa miradi,” amesema Ulega.
Ameeleza kuwa hatua hizo zimeendelea kuongeza uwezo wa Wizara kufuatilia maendeleo ya wakandarasi wanawake na kuweka mazingira bora yatakayochochea ushiriki mkubwa zaidi wa wanawake katika sekta ya barabara na ujenzi nchini.

Comments
Post a Comment