Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amesema kati ya waathirika hao, watoto ni 60, wanawake 96 na wanaume 4.
Ameeleza kuwa waathirika 126 waliokolewa ndani ya nchi na 34 waliokolewa kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Bahrain, India, Malaysia, Misri, Oman, Syria na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Katika hatua nyingine, jumla ya watuhumiwa 57 walikamatwa, ambapo 45 kati yao wamefikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea kusikilizwa katika mikoa mbalimbali nchini, huku 12 wakiendelea kuchunguzwa na vyombo vya dola.
Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa wadau wa haki jinai kupitia mafunzo maalum yaliyotolewa kwa washiriki 314 katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kagera, Mwanza na Singida. Mafunzo hayo yanalenga kuboresha utambuzi wa waathirika, upelelezi na uendeshaji wa mashitaka kwa ufanisi zaidi.
Vilevile, elimu kwa umma imeendelea kutolewa kupitia mitandao ya kijamii, redio, televisheni, makongamano, semina na maonesho mbalimbali, ambapo jumla ya wananchi 19,076 walifikishwa na kufikiwa na elimu hiyo kuhusu madhara ya usafirishaji haramu wa binadamu.
Katika kuimarisha upokeaji wa taarifa, Serikali imeanzisha Kituo cha Kitaifa cha Kupokea Taarifa za Uhalifu wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu, ambapo wananchi wanahimizwa kutoa taarifa kwa kupiga simu bure namba 195.
Pia, Serikali imeanzisha Ofisi ya Kanda ya Dar es Salaam itakayohudumia mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Mtwara, Pwani na Tanga, sambamba na kuendelea na ujenzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa TIPMIS ambao umefikia asilimia 50 ya utekelezaji wake.
Katika sekta ya huduma kwa waathirika, Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba salama mkoani Dodoma ambao umefikia asilimia 60, huku ikipanga kujenga nyumba nyingine jijini Dar es Salaam katika mwaka wa fedha 2026/27.
Serikali imetenga Shilingi bilioni 2.76 kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, ikijumuisha ujenzi wa nyumba salama, kuimarisha operesheni za uokoaji, kutoa elimu kwa umma pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Comments
Post a Comment