Serikali yaleta Mwelekeo Mpya Ithibati; Wanahabari Wakongwe kurejeshwa rasmi katika Tasnia ya Habari
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeandaa mwongozo maalumu wa kisheria utakaowezesha wanahabari wakongwe waliokuwa wameathiriwa na mfumo wa ithibati kurejea rasmi katika tasnia ya uandishi wa habari.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakatu akiwasilisha bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27.
hatua hiyo inalenga kuimarisha ushiriki wa wanahabari wenye uzoefu mkubwa katika sekta ya habari nchini.
“Wizara kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari tumeandaa mwongozo maalumu wa kisheria utakaowezesha wanahabari wakongwe walioathiriwa na mfumo wa ithibati kurejea katika mfumo.”. Amesema
Amefafanua kuwa mwongozo huo umeandaliwa kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, yenye lengo la kuimarisha na kudhibiti taaluma ya uandishi wa habari kwa kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, wanahabari wakongwe hawatatazamwa tu kwa vigezo vya kitaaluma, bali pia uzoefu wao, weledi na mchango wao katika tasnia ya habari.
Ameeleza kuwa mchakato huo utahusisha tathmini maalumu itakayojikita katika historia ya kazi, mchango wa kitaaluma pamoja na ufuataji wa maadili ya uandishi wa habari.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ushiriki wa wanahabari wenye uzoefu katika sekta hiyo, kuboresha ubora wa taarifa kwa umma na kuimarisha tasnia ya habari yenye weledi, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria, huku ikichangia kujenga mfumo wa habari unaoaminika na wenye tija kwa jamii.



Comments
Post a Comment