SERIKALI imetangaza mikakati mipya ya kuimarisha sekta ya elimu, sayansi na teknolojia nchini, ikilenga kuongeza ubora wa elimu, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi pamoja na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha elimu na ubunifu katika ukanda wa Afrika.
Mikakati hiyo imetangazwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Mei 7, 2026 Bungeni jijini Dodoma.
Prof. Mkenda amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Umataifishaji wa Elimu wa mwaka 2025 wenye lengo la kuongeza ufanisi katika kuandaa wahitimu wenye maarifa, stadi na umahiri unaokidhi mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Amesema mkakati huo pia utaimarisha mitaala na mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kuvutia wanafunzi na wanataaluma kutoka nje ya nchi pamoja na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za elimu za ndani na nje ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, Serikali imeandaa Mkakati wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika elimu na mafunzo ili kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya elimu nchini.
Prof. Mkenda amesema Serikali pia imekuja na Mkakati wa Kitaifa wa Ugharamiaji na Motisha katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu utakaosaidia kuimarisha mifumo ya ufadhili wa tafiti, ubunifu na teknolojia kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amesema Wizara imeandaa Mkakati wa Usawa wa Kijinsia wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30 utakaotekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ili kuimarisha usawa wa kijinsia na elimu jumuishi nchini.
“Wizara imekubaliana na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kutafuta fursa na rasilimali kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa elimu, sayansi na teknolojia ikiwemo suala la umataifishaji elimu,” amesema Prof. Mkenda.
Sambamba na hilo, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa Mfumo wa Takwimu wa Sekta ya Elimu (ESMIS) ambao umeunganisha mifumo mbalimbali ya elimu chini ya wizara mbalimbali na kuwezesha upatikanaji wa takwimu zote za sekta katika eneo moja, huku ukusanyaji wa takwimu za elimu za mwaka 2026 ukiwa tayari umeanza.

Comments
Post a Comment