SERIKALI imezindua mkakati mpya wa kupanua elimu ya amali na mafunzo ya ufundi nchini huku ikilenga kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri na kupata ajira katika soko la ndani na kimataifa.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Mei 7, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema serikali itadahili wanafunzi 374,000 katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na mwaka uliopita.
“Ongezeko la udahili wa wanafunzi wa vyuo vya ufundi kutaongeza idadi ya vijana wenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa,” alisema Prof. Mkenda.
Katika kuimarisha sekta hiyo, serikali itasajili vyuo 263 vya elimu ya ufundi, mafunzo ya ufundi stadi pamoja na shule za sekondari za amali, hatua itakayoongeza upatikanaji wa mafunzo ya vitendo kwa vijana wengi zaidi nchini.
Prof. Mkenda amesema serikali imeamua kuelekeza nguvu zaidi katika elimu ya vitendo kutokana na mahitaji makubwa ya soko la ajira la sasa.
“Ulimwengu wa sasa unahitaji zaidi vitendo kuliko nadharia, hivyo walimu wa amali ndio msingi wa kuandaa vijana wenye uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo,” alisisitiza.
Aidha, serikali itadahili walimu tarajali 1,200 wa amali na kuendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi, shule za amali, mabweni, maabara, maktaba pamoja na vyuo vya kisasa vya polytechnic katika mikoa mbalimbali nchini.
Hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya wahitimu wenye ujuzi wa kiufundi na kuifanya elimu ya amali kuwa mhimili mkubwa wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya Taifa.


Comments
Post a Comment